Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4510

NEMC KUONDOA MINARA YA SIMU KWENYE MAKAZI YA WATU

$
0
0
Baraza la Taifa la Hifadhi  na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesema linaanza kupitia miradi mbalimbali, ikiwemo minara ya mawasiliano ya simu iliyojengwa  kwenye makazi ya watu.
Lengo ni kuihamisha ili kudhibiti athari za mazingira na afya kwa binadamu katika maeneo husika.  Kazi hiyo itafanywa kwa kushirikiana na halmashauri zote nchini.
Kwa kuanzia, baraza hilo linatoa mafunzo kwa maofisa mazingira wa halmashauri Kanda ya Kaskazini yenye mikoa ya Manyara,Tanga na Arusha. Mafunzo hayo ni ya  kuwezesha mkakati huo wa kupitia miradi mikubwa.
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Boniventure Baya, alisema ujenzi wa minara ya  mawasiliano ya simu, unaenda kwa kasi nchini,  ambapo kwa sasa imefikia  15,000 na ipo karibu na makazi ya watu.
Alisema hali hiyo inatishia mazingira na afya za wananchi, kutokana na mionzi inayoleta athari za kibailojia.
Alisema baada ya kubaini hilo,  minara iliyo katika makazi ya watu, itaondolewa na kupangwa katika maeneo ambayo hayatakuwa na athari kwa jamii.
Baya alisema  kuwa miradi ya maendeleo imekuwa ikiongezeka kwa kasi, kutokana na mahitaji makubwa, hivyo ni wajibu wa NEMC kuhakikisha  haiathiri mazingira, hasa katika maeneo ya makazi ya watu.
Mkurugenzi wa Idara ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM), Ignace Mchallo, alisema kupitia mafunzo hayo, maofisa hao mazingira wataweka mikakati kudhibiti athari zinazotokana na ujenzi wa miradi.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Lameck Noah alitaka NEMC kuhakikisha  inakabiliana na changamoto za athari za mabadiliko ya tabia nchi, ambayo yamekuwa yakiathiri zaidi mazingira.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4510

Trending Articles