
Kesi hiyo ilifunguliwa dhidi ya Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kutokana na kauli aliyoitoa Pinda bungeni, Juni 20, mwaka jana wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo, wakidai ni amri kwa vyombo vya utekelezaji wa sheria kuwapiga wananchi wakati wa vurugu.
Katika uamuzi, jopo la majaji watatu, Jaji Kiongozi Fakih Jundu, Agustine Mwarija na Dk Fauz Twai, lilitupilia mbali kesi hiyo kwa kuwa waliofungua hawana haki kisheria.
Iliamuriwa pia kwamba walikosea taratibu za ufunguaji wa kesi kama hizo, kwa kuwa walikiuka amri na kanuni zinazoongoza Mashauri ya Madai (CPC).
Mahakama ilisema anayepaswa kufungua kesi ni mtu aliyeathirika na kauli iliyotolewa na mlalamikiwa, na si mashirika, kwa kuwa kauli ya mlalamikiwa haikuathiri mashirika hayo, yaliyofungua kesi.
Ilifafanua kuwa mtu aliyeathirika na kauli iliyotolewa bungeni, anaweza kuwasilisha malalamiko yake kwa Spika kwa mujibu wa Kanuni ya 71 (1) ya Bunge, lakini siyo mashirika, isipokuwa yanaweza kufungua kesi mahakamani kama kauli imeyaathiri.
Katika madai yao TLS na LHRC, waliiomba Mahakama, itamke kuwa kauli hiyo ni kinyume cha Katiba na imwamuru Pinda aifute hadharani.
Hata hivyo, mawakili wa Pinda walisema Pinda analindwa na Katiba Ibara ya 100 (1) na (2), ambazo zinamkinga mbunge kushitakiwa au kufunguliwa shauri la madai mahakamani kwa jambo lolote alilolisema, au alilolitenda, au aliloliwasilisha bungeni kwa njia ya maombi, muswada au hoja.