Hali ya usalama nchini Kenya ni tete kutokana na mfululizo wa mashambulizi yaliyofanyika jana na juzi katika Mji wa Mpeketoni na kusababisha vifo vya watu wapatao 60.
Ikiachwa shambulizi la juzi ambalo inasadikiwa kundi la wanamgambo wa Al Shabaab ndilo lilitekeleza kwa kuua watu 48 katika eneo la Mpeketoni karibu na Mji wa Lamu, shambulizi lingine limetokea jana katika eneo hilo lililoko pwani ya Kenya na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 10.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi hiyo, Joseph Ole Lenku, washambuliaji waliharibu kituo cha mawasliano cha Safaricom kabla ya kutekeleza uhalifu huo wakilenga kuzuia wakazi kuwasiliana na watu wa nje .
Polisi nchini Kenya, imesema , washambuliaji hao walitekeleza uhalifu huo usiku kucha wakifyatua risasi hovyo kwa wananchi ambao wengi wao walikuwa wakiangalia mechi ya kombe la dunia.
Taarifa zinasema kundi la Al Shabaab limekiri kufanya mashambulizi hayo kwa kuliambia Shirika la Habari la Reuters kwamba operesheni yao ya mashambulizi itaendelea nchini Kenya.