Mbunge wa Ukerewe, mkoani Mwanza, Salvatory Machemli ameachiwa huru na Mahakama baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka ya uchochezi yaliyokuwa yakimkabili.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ukerewe, Faustine Kishenyi.
Hakimu Kishenyi alisema mahakama imeridhika mshitakiwa hana hatia baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha kosa lake.
Alisema mbali ya Polisi kushindwa kuwasilisha vielelezo mahakamani kama ilivyo katika hati ya mashitaka, pia ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka unaonekana kuzingatia zaidi maslahi yake; hivyo haujitoshelezi kumtia mshitakiwa hatiani.
Kwa mujibu wa hakimu, upande wa mashitaka umeshindwa kuwasilisha CD iliyochukuliwa wakati mshitakiwa akitenda kosa huku polisi watatu wakiwa ndio pekee wametoa ushahidi dhidi ya mshitakiwa.
Amesema ushahidi uliothibitishwa na shahidi kutoka nje ya jeshi hilo ambalo ndio linadai kulengwa, unaonekana kuwa na maslahi ya upande mmoja hivyo hauwezi kutumika kumtia hatiani mshitakiwa.
Awali ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Samwel Onyango kuwa Machemli (39) alitenda kosa la uchochezi Oktoba 23 mwaka 2011 wakati anahutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Nyamanga kisiwani Ukara.
Ilidaiwa Machemli kwa makusudi alichochea wananchi wazuie shughuli za polisi na hata kuwashambulia wakienda katika maeneo yao kutafuta wahalifu.