Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk, Richard Sezibera ameasa wabunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) kuacha tabia ya kudhalilisha Baraza la Mawaziri.
Amesema baraza hilo ndicho chombo kinachotoa ushauri kwa wakuu wa nchi wanachama kuhusu masuala ya jumuiya hiyo. Aidha ametoa rai kwa wabunge wa bunge hilo kuacha kudhalilisha Bunge na jumuiya kwa kulifanya kuwa sehemu ya migogoro isiyoisha.
Ametaka waache tabia ya kudharau utendaji kazi katika ofisi mbalimbali zilizopo ndani ya jumuiya hiyo.
Sezibera aliyasema hayo jana ndani ya Bunge wakati alipokuwa akitoa hoja wakati wa kujadiliwa na hatimaye kupitishwa kwa bajeti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambayo imepita bila kupingwa.
Alisema si busara kwa wabunge wa EALA kudhalilisha Baraza la Mawaziri ambao ndio wanaowashauri wakuu wa nchi na kuongeza kuwa ni vyema wabunge hao wakahakikisha wanasimamia masuala yanayohusu nchi wanachama wa jumuiya hizo.
Waziri wa EAC kutoka Uganda, Shem Bagaine alisema wanatafuta vyanzo vya fedha vitakavyokidhi bajeti ya jumuiya hiyo.
Alisisitiza, Agosti m waka huu watapeleka suala hilo kwenye Kikao cha Baraza la Mawaziri kujadili mapendekezo ya kukata asilimia moja ya kodi zote za bidhaa za nchi za EAC na ombi hilo likipitishwa litaweza kupunguza utegemezi wa bajeti kwa nchi wahisani. Bajeti iliyopitishwa na Bunge hilo ni dola za Marekani 124,169,625 .