Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4529

MTOTO MCHANGA APONA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA UKIMWI...

$
0
0
Mtoto aliyezaliwa na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi, amepona baada ya kutibiwa, watafiti wameeleza.
Mtoto huyo wa Mississipi nchini Marekani, kwa sasa ana miaka miwili na miezi sita na amethibitika kuishi bila virusi hivyo yapata mwaka sasa.
Majaribio zaidi yamepangwa kufanywa, kuona kama tiba hiyo inafaa kutumika kwa watoto wengine wachanga, wenye maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi.
Watafiti waliofanikiwa kumtibu mtoto huyo, wameeleza kuwa tiba hiyo inaweza kubadilisha hali ya hatari inayowakabili watoto wachanga, ambao wanaendelea kutibiwa na kujikuta wanaponyeshwa maambukizi ya virusi hivyo.
"Matokeo haya yanathibitisha kuwa Ukimwi unaweza kutibika kwa watoto wachanga,” alisema Dk Deborah Persaud wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Johns Hopkins kilichoko Baltimore.
Alisema hayo wakati akiwasilisha utafiti wake katika mkutano uliokuwa unazungumzia masuala ya maambukizi ya HIV na fursa iliyopo ya kupambana nayo.
Alisema iwapo mtoto huyo ataendelea kuwa na afya njema, litakuwa tukio la pili kwa mtu mwenye Ukimwi kutibiwa na kupona baada ya lile la mwaka 2007, ambapo Timothy Brown aligundulika kuponywa maradhi hayo ambayo kwa sasa hayana tiba.
Virusi vya Ukimwi alivyokuwa navyo, viliponyeshwa kwa dawa alizokuwa anatumia wakati anapata matibabu ya saratani ya damu, ambayo ilichangia kinga zake kuwa chini na kuathiri chembehai mbalimbali za mwili.
Lakini matibabu yaliyotumika kwa mtoto huyu, yalielezwa kuwa tofauti na ya Brown; kutokana na kuhusisha kwa kiasi kikubwa dawa zinazotumika kwa sasa katika tiba za majaribio kwa watoto wenye maambukizi.
Mtoto huyo alizaliwa vijijini na mama ambaye alipimwa wakati wa ujauzito na kugundulika kuwa na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi.
Kwa vile mama huyo hakuwa amepata matibabu yoyote ya kumkinga mtoto wakati wa ujauzito, madaktari walitambua kuwa mtoto angezaliwa akiwa na uwezekano mkubwa wa maambukizi.
Hivyo, hatua za kumhamisha mtoto kwenda Chuo Kikuu cha Mississipi baada ya saa 30 kupita tangu kuzaliwa kwake, ilifanywa na alianzishwa matibabu tofauti ya aina tatu  maalumu kwa ajili tiba za majaribio kwa watoto wenye Virusi Vya Ukimwi hata kabla ya vipimo vya maabara kuthibitisha kuwa amezaliwa na maambukizi.
Baada ya kumwanzisha matibabu chini ya uangalizi wa karibu wa Dk Hannah Gay, ambaye ni bingwa wa magonjwa ya Ukimwi, kidogo kidogo kinga za mtoto huyo zilianza kuimarika na maambukizi hayo kutoweka alipofikisha umri wa siku 29.
Mtoto huyo aliendelea na matibabu ya mara kwa mara kwa miezi 18 na baadaye aliacha kwa miezi 10 na kupelekwa kwa  mama yake ambaye alikiri kuwa katika kipindi alichokaa naye, hakuwahi kumpeleka hospitalini.
Baada ya mtoto huyo kurejeshwa kwa Dk Gay, aliamuru apimwe damu yake tena kuona kama dawa alizotumia zimemsaidia na ndipo kipimo cha kwanza hakikubaini virusi.
Alipochukuliwa vipimo vingine chini ya uangalizi wa matabibu waliobobea katika masuala ya Ukimwi, ilibainika kuwa hakuwa na maambukizi tena.
"Baadaye nilitambua kuwa nilikuwa nashughulika na suala ambalo si la kawaida,” alisema Dk Gay na kuongeza kuwa baadaye damu ya mtoto huyo ilipimwa tena na ikabainika hakuwa na maambukizi kwenye damu yake.
Madaktari walishauri mtoto huyo asiendelee kutumia dawa tena ila awe chini ya uangalizi wao.
“Ni jambo la kufurahisha, kuwa tumejifunza zaidi juu ya kinga za mtoto mchanga, namna zinavyotofautiana na kinga za mtu mzima na namna watoto wachanga walivyo rahisi kutibiwa maradhi ya Ukimwi,” alisema Dk Rowena.
Dk Johnston ni Makamu wa Rais na Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Ukimwi, ambaye  alisaidia fedha kwa ajili ya matibabu ya mtoto huyo.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4529

Trending Articles