Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4529

SERUKAMBA AWEKWA KITI MOTO MBELE YA KINANA

$
0
0
Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba amejikuta katika wakati mgumu kwenye mkutano wa Halmashauri ya CCM wilaya ya Kigoma Mjini, baada ya kudaiwa na baadhi ya wajumbe kwamba hana ushirikiano na wenzake.
Wamemshutumu kwamba tangu alipochaguliwa kuwa mbunge, hakushukuru wananchi.
Serukamba alikumbwa na adha hiyo, mbele ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ambaye alimpa nafasi ya kujitetea.
Katika maelezo yake kwenye mkutano huo, Serukamba alikiri kutofanya mikutano hiyo.
Lakini, alisisitiza kwamba, amekuwa na bahati mbaya hata akifanya jambo lolote zuri mkoani humo, hatambuliwi wala kupongezwa.
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Kata wa eneo la Mwanga Mjini, wilayani hapo, Shiza Athuman, alisema hali ya kisiasa ya chama hicho, inazidi kuwa mbaya wilayani humo.
Alidai hali hiyo inatokana na mbunge huyo, kutofanya mikutano ya mara kwa mara na wananchi, kuwaelezea matatizo ya wapinzani ndani ya vikao vya halmashauri.
"Ndugu Kinana, unavyomuona mbunge wetu hapo tangu achaguliwe hajawahi kushukuru wananchi, lakini pia haingii hata kwenye vikao vya halmashauri ili kujua nini kinaendelea kuhusu maendeleo ya wananchi," alisema Athuman.
Alisema katika wilaya hiyo, kwa sehemu kubwa kikao cha halmashauri ya manispaa, kimetawaliwa na madiwani wa upinzani, ikiwa ni pamoja na meya wa manispaa hiyo.
"Ndio maana wananchi wana malalamiko mengi na matatizo, lakini kwa kuwa mbunge wetu hahudhurii vikao, anawaachia watu hawa wanafanya uamuzi," alisema.
Aidha, Athuman alihoji juu ya namna mbunge huyo alivyotumia fedha zinazotolewa na Bunge kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za wabunge majimboni, kwa kuwa hadi sasa katika jimbo hilo hakuna ofisi  wala dalili ya kujengwa kwake.
Kinana alimtaka Serukamba ajibu na katika majibu alisema, "Ni  kweli sijafanya mikutano, lakini kuhusu kushukuru nakiri kuwa sikwenda maeneo yote, nilishukuru katika yale maeneo makubwa, ila jamani kumbukeni mwenzenu nilikuwa na matatizo ya kesi ya uchaguzi."
Alisema muda wake mwingi, aliutumia katika kushughulikia kesi hiyo, ambayo hata hivyo, cha kushangaza baadhi ya watu ndani ya chama hicho, walikuwa wakisubiri ashindwe  washerehekee.
Kuhusu fedha za ujenzi wa ofisi ya mbunge, Serukamba alisema kamwe hawezi kula fedha za ujenzi wa ofisi ya Bunge.
"Siwezi kula fedha za ujenzi wa ofisi, kwanza fedha hizi huu ni mwaka wangu wa nane wa ubunge, sijaziona wala wabunge wenzangu, ni majimbo mawili tu ndio yamejengewa," alisema.
Alisema kila mwezi huwa anapatiwa na Bunge Sh milioni 42 kwa ajili ya Mfuko wa Jimbo, ambazo hajawahi kula hata senti tano na huzikabidhi kwenye mfuko wa halmashauri ziendeleze miradi ya ujenzi wa madawati kwa kuwa ni tatizo kubwa wilayani hapo pamoja na ujenzi wa matundu ya vyoo shuleni.
Aidha, alisema katika wilaya hiyo, akiwa kama mbunge ametoa mchango mkubwa katika masuala ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara za mitaa kwa kiwango cha lami.
"Yote haya nimechangia mimi kama mbunge, lakini cha kushangaza utasikia watu wakisimama kwenye majukwaa, anapongezwa Rais Jakaya Kikwete, mbunge anaachwa, hii ni kawaida ya mkoa huu, mimi siwezi kujitangaza ila nitajitangaza kwa kazi ninazofanya," alisisitiza.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4529

Trending Articles