Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4503

MAGUFULI AAGIZA MATENGENEZO YA HARAKA DARAJA LA MPIJI

$
0
0
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli ametaka watendaji wa Wakala wa Barabara (Tanroads), kuharakisha matengenezo ya barabara karibu na Daraja la Mpiji ili kurejesha mawasiliano kati ya Dar es Salaam na Pwani.
Mawasiliano ya barabara kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo, yalikatika  juzi, kutokana na barabara hiyo kubomolewa na maji katika Daraja la Mpiji, mpakani mwa mikoa hiyo kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha sehemu mbalimbali nchini.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya kukatika kwa barabara hiyo, Dk Magufuli aliwaagiza watendaji hao, kuhakikisha wanafanya kazi mchana na usiku hadi  barabara hiyo muhimu na yenye kupitisha magari mengi, ifunguliwe mapema iwezekanavyo.
Magufuli pia aliagiza kuahirishwa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Tanroads, ambao ulipangwa kuanza kesho mjini Tanga hadi itakapopangwa baadae.
Alisema hatua ya kuahirishwa kwa mkutano huo, ni kutoa nafasi kwa watendaji wa wakala  kubaki katika vituo vyao vya kazi hadi hali ya mvua zinazoendelea itakapotulia.
Akizungumzia hali katika eneo hilo la Mpiji, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mussa Iyombe, alisema kilichozolewa na maji ni sehemu ya barabara na siyo daraja lenyewe la Mpiji.
Dk Magufuli alihadharisha kuhusu shughuli za uchimbaji wa mchanga, zinazofanywa karibu au chini ya madaraja  katika maeneo mengi nchini, kuwa zimekuwa chanzo cha mito kuhama kutoka katika njia yake ya asili na kubomoa barabara.
"Kama mnavyoona daraja lenyewe ni zima na lina uwezo mkubwa wa kupitisha maji, lakini mto umehama kutokana na uharibifu wa mazingira," alisisitiza Dk Magufuli.
Daraja la Mpiji lilifunguliwa rasmi  Julai 2005. Tanroads  kwa kushirikiana na kampuni za ujenzi za SKOL na Estim Construction Company Limited, zote za Dar es Salaam, wameanza kazi za kurekebisha sehemu hiyo.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4503

Trending Articles