![]() |
Wajumbe Bunge Maalum la Katiba wakipiga kura. |
Aidha, uamuzi huo pia uliamuliwa kwa kura ya wazi na siri na matokeo yalikuwa……(Hapa pa kuweka kura zitakapotoka).
Hatua hiyo ilitokana na pendekezo la Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalumu kuwa kura zote zitumike, lakini katika michango ya wajumbe waliochangia pendekezo hilo, waligawanyika.
Katika mgawanyiko huo, waliopendelea kura ya wazi, hawakupingawanaotaka kura ya siri.
Lakini, waliopendekeza kura ya siri, walipinga namna yoyote ya kupiga kura ya wazi.
Baadhi ya wajumbe, akiwemo John Mnyika, Mbunge wa Ubungo, alipendekeza kura ya siri itumike katika baadhi ya mambo ambayo hayana mvutano.
Katika hoja yake, alidai hakuna mahali popote duniani ambako kura zote mbili hutumika na ikianza Tanzania, itakuwa ni kioja.
Hata hivyo, waliochangia hoja hiyo akiwemo Sixtus Mapunda, mjumbe kutoka Kundi la 201, aliunga mkono hoja ya kura zote zitumike na alifafanua kuwa, si ajabu kwa Tanzania kuanzisha mfumo huo.
Mjumbe Goodluck ole Medeye, alisema kura mbili hutumika na alitoa mfano wa Bunge la Italia kuwa hutumia kura mbili tangu 1970 na katika Mkutano wa Shirika la Posta Duniani mwaka 1964, ilitumika kura mbili kuiondoa nchi ya Afrika Kusini.
Hata hivyo alifafanua kuwa, tofauti ya kura hizo na inayopendekezwa, hiyo ya zamani wajumbe hupiga kura mara mbili, kwanza ya wazi na pili kura ya siri kuthibitisha walichoamua wazi na kura ya siri ndiyo huwa ya uamuzi.
Alisema kwa kura inayopigwa sasa, wajumbe wataamua iwe ya siri au ya wazi na zitapigwa pamoja kwa wanaotaka siri, kupiga kura ya siri na kwa wanaotaka wazi wapige ya wazi.
Kutokana na suala hilo kugawa Bunge Maalum katika makundi mawili makubwa, wanaotaka siri na kupinga wazi na wanaotaka wazi bila kupinga siri, Mwenyekiti wa Bunge Maalum, Samuel Sitta aliteua kamati ya muda ya maridhiano ili kupata muafaka.
Kamati hiyo kwa mujibu wa mmoja wa wajumbe wake, Vuai Ali Vuai, ambaye ni mjumbe kutoka kundi 201, ilikaa juzi kuanzia saa 2:00 usiku mpaka saa 8:00 usiku bila kufikia muafaka.
Baada ya hapo, waliamua kukutana jana asubuhi kuanzia 4:00 asubuhi mpaka saa 6:00 mchana, napo hawakukubaliana na wakaamua kukutana tena saa 8:00 mchana mpaka saa 9:00 alasiri, wakaamua kura zote mbili, za wazi na siri, zitumike.
Mjumbe mwingine wa kamati hiyo ya muda, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema katika mkutano wa Kamati ya Muda ya Maridhiano, suala la utata lilikuwa kwamba wanaokubali kura ya wazi, hawakwazwi na kura ya siri, lakini wanaokubali kura ya siri, wanakwazwa na kura ya wazi.
Alisema suala hilo ni dogo, lakini wenzao kwa maana ya CCM, wamekuwa na msimamo na ili rasimu ya Katiba ijadiliwe na mchakato uende mbele, basi kura zote za siri na wazi zipigwe, lakini si nzuri zitaleta vikwazo.
Mjumbe Mnyika wa Kamati hiyo ya muda, alimnukuu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere katika kitabu chake cha Tujisahihishe, aliposema wachache husikilizwa lakini wengi huamua na wachache wanapotaka kuamua, kwa kuwa wazo zuri daima hutoka kwa mtu mmoja, wanapaswa kushawishi wengi wakubaliane nao.
“Sasa tumekubaliana katika uamuzi wa leo, kila mmoja aamue iwe wazi au siri…tumekubaliana ili tupige hatua mbele, tukubali hilo.
“Lakini kwa ajili ya kuweka wazi kuwa tumekubaliana kutokukubaliana, sisi (Chadema), tumekubaliana kupiga kura ya wazi ya hapana,” alisema Mnyika, ambaye alimwakilisha Mjumbe, Freeman Mbowe, Mbunge wa Hai, ambaye alipata udhuru kutokana na msiba.
Mjumbe mwingine wa kamati hiyo ndogo, Askofu Mkuu mstaafu Donald Mtetemela, alisema katika kikao chao aliona kulikuwa na nia njema na kubwa kila mmoja aliona umuhimu wa mchakato huo kwenda mbele.
Baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalumu, Pandu Ameir Kificho, kuhitimisha hoja ya Azimio la Bunge Maalumu la Katiba, kuhusu kura zote za siri na wazi kutumika, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta alitangaza utaratibu.
wanaotaka kuamua azimio hilo lipite au lisipite kwa kura ya wazi, wakiitwa jina waseme ‘Ndio’ au ‘Hapana’ na kura hiyo itarekodiwa.
Kwa wanaotaka kuamua kwa siri, waliitwa mbele na kuchukua karatasi ya kura yenye neno ‘Ndio’ na ‘Hapana’, ambapo mjumbe alitakiwa kuweka alama ya Vema (V) katika neno analokubaliana nalo.