![]() |
Baadhi ya makahaba wenye umri mdogo wakiwa kwenye mawindo yao. |
Mji uliotajwa kuwa na watoto hao kutoka nchini China ni wa Guangzhou.
Imeelezwa wamekuwa wakinyang'anywa hati zao za kusafiria na kuwataka watoe dola za Marekani 8,000 kuzigomboa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu wizara yake nchini China.
Alisema mwezi uliopita alipata mwaliko nchini humo na kubaini kuwapo biashara hiyo katika mji wa Guangzhou.
Alisema kutokana na taarifa hizo, ameitaarifu Wizara ya Mambo ya Ndani kuunda timu kwenda nchini humo na pia kubaini wanaoendesha biashara hiyo kuhakikisha inakomeshwa mara moja.
Alisema imebainika wapo baadhi ya Watanzania wanakwenda China kwa kutumia nyaraka bandia hati za kusafiria za nchi nyingine.
Hata hivyo alisema siyo kwamba Watanzania walioko mji huo wote wanaendesha biashara haramu au hawakai kihalali kwa kuwa wapo wengi na wameanzisha ofisi ya diaspora wakiishi kihalali.
"Lakini wapo walioanzisha biashara hiyo na kuvunja heshima ya binadamu na nchi kwani kuna msichana mmoja alifariki kwa kuuawa nchini humo wiki iliyopita na upelelezi unaendelea," alisema Membe.
Alisisitiza kuwepo Watanzania wanaoishi nje ya nchi zaidi ya milioni tatu na wengi wao wakiishi vizuri. Lakini wengine wanashutumiwa kwa kutoitendea haki nchi kwa kufanya vitendo visivyo halali.
Aliomba Watanzania hususan watoto wadogo wa kike kutorubuniwa kupelekwa nje kwa ahadi za kupata pesa na maisha mazuri.
Membe alisema ni vyema kutii kanuni na sheria kupunguza wanaopata matatizo ikiwa ni pamoja na kukataa kutumika kubeba dawa za kulevya kwa kupewa fedha kidogo ambapo wakati mwingine husababisha kifo.
Alisema Oktoba mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete anatarajia kufanya ziara China na ni mategemeo kwamba matatizo yaliyojitokeza wakati wa ziara yake yatakuwa yamefanyiwa kazi.
Wakati huo huo Waziri Membe alisema nchi 10 zinatarajia kufungua balozi zake nchini. Miongoni mwake ni Australia, Kuwait na Comoro.
Alisema kwa sasa nchi hizo zinatafutiwa viwanja kwa ajili ya balozi hizo pamoja na maeneo ya kuishi jambo ambalo litaongeza ajira na mzunguko wa fedha.