Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4529

MALALAMIKO YA TANZANIA BARA, ZANZIBAR KUWEKWA HADHARANI...

$
0
0
Jaji Joseph Warioba.
Mweyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, ametaja malalamiko 10 ya kila upande wa Muungano, ambayo yanatishia kuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ikiwemo Serikali ya Tanganyika kuvaa koti la Serikali ya Muungano ambalo linaisaidia Tanganyika zaidi kuliko Zanzibar.

Taswira hiyo imeifanya Tanganyika kuwa Tanzania na Watanganyika ndio wamekuwa Watanzania na Wazanzibari wamebaki kuwa Wazanzibari.
Wazanzibari pia wanalalamika mambo ya Muungano yamekuwa yakizidi kuongezeka na kuathiri uhuru wa Zanzibar na kufifisha hadhi ya Zanzibar. Wanalalamika pia kuvunjwa kwa makubaliano ya Hati ya Muungano kwa kuificha sura ya Tanganyika katika muundo Serikali ya Muungano.
Wanalalamika pia kumuondoa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Serikali ya Muungano na kutokuwepo kwa uwazi wa mapato na matumizi ya fedha za Serikali ya Muungano.
Warioba pia alisema Wazanzibari wanalalamika kutoanzishwa kwa akaunti ya fedha ya pamoja, kuwepo kwa mkanganyiko wa ugawaji wa mapato na jinsi ya kuchangia gharama za uendeshaji wa shughuli za Muungano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar.
Malalamiko mengine ni kuwepo kwa uchumi  wa aina mbili tofauti unaoshindana katika nchi moja, Zanzibar kutoshirikishwa kikamilifu na Serikali ya Muungano katika msuala ya kupata misaada na mikopo kutoka nje, hata kama Rais wa Muungano anatoka Zanzibar na wanalalamika kuwa viongozi wakuu wa Zanzibar, wanachaguliwa Dodoma na sio Zanzibar kwenyewe.
Lalamiko la mwisho la Wazanzibari ni kuwa kuna baadhi ya mambo yamefanywa kuwa ya Muungano kupitia kutungwa kwa sheria na Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa mambo yasiyo ya Muungano na baada ya hapo mambo hayo kupata hadhi ya Muungano.
Watanzania bara kwa upande wao, wanalalamika kuwa Zanzibar imekuwa nchi huru, ina bendera yake, ina Wimbo wake wa Taifa, ina serikali yake na imebadili Katiba yake ili kujitambua kama nchi.
Zanzibar imebadili masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, ambayo inasema sheria za Muungano zinazotungwa na Bunge la Muungano zitumike sehemu yote ya Muungano, badala yake Katiba ya Zanzibar inaelekeza kuwa ili sheria itumike Zanzibar, ni sharti ipelekwe mbele ya Baraza la Wawakilishi.
“Maana yake Katiba ya Zanzibar iko juu  ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano,” alisema Warioba na kutaja lalamiko lingine kuwa ni  Zanzibar kutunga sheria kuhusu fedha, ambalo ni suala lililo kwenye madaraka ya Muungano.
Malalamiko mengine ni Zanzibar kutunga Katiba ambayo imechukua madaraka ya Rais yaliyomo katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano yanayoeleza kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano ana madaraka ya kugawa maeneo ya nchi ya kiutawala.
Lakini mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, yameitambua Zanzibar kama  nchi na yanampatia mamlaka Rais wa Zanzibar kuigawa nchi katika maeneo ya kiutawala.
Wabara pia wanalalamika  Katiba ya Zanzibar, inaeleza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi mbili, lakini Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaeleza kwamba Tanzania ni nchi moja.
Masharti ya kikatiba yaliyowekwa na Katiba ya Zanzibar  kuhusu mchango wa Zanzibar katika uendeshaji wa mambo ya Muungano yanapingana na masharti ya Katiba ya Muungano.
Pia alisema muundo wa Muungano uliopo umepoteza utambulisho wa kihistoria wa Tanganyika na fursa ya watu wa Tanganyika kutetea maslahi ya ndani ya Muungano.
Wananchi wa Tanzania Bara pia wanalalamikia kutokuwa na haki ya kumiliki ardhi Zanzibar, wakati wenzao wa upande wa Zanzibar wana haki ya kumiliki ardhi Tanzania Bara.
Pia wabunge wa Zanzibar huchangia mijadala kwa mambo yasiyo ya Muungano na ambayo kwa hakika ni mambo ya Tanganyika wakati wabunge wa Tanganyika hawana nafasi ya kuchangia katika Baraza la Wawakilishi kwa mambo yasiyo ya Muungano yanayohusu Zanzibar.
Lalamiko la mwisho la Wabara ni kwamba kwa mujibu wa Sheria  ya Mzanzibari ya mwaka 1985, Watanzania ambao ni Watanzania wa Bara hutakiwa kutimiza sifa maalumu, ili  kupata haki za kiraia huko Zanzibar, ilhali Mzanzibari hupata haki  ya kiraia wakati wowote na popote katika ardhi ya Tanganyika.
Haki hizo za kiraia ni pamoja na kugombea uongozi na kupiga kura.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4529

Trending Articles