Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4510

KARDINALI PENGO AICHAMBUA KATIBA YA ZANZIBAR, ASEMA IMEKOSEWA...

$
0
0
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Wakati maandalizi ya Bunge Maalumu la Katiba yakiendelea, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amesema Katiba ya Zanzibar imekosewa na kosa hilo linahatarisha umoja wa Taifa.

“Kwa sababu kosa hilo (katika Katiba ya Zanzibar) limefanyika, basi na sisi tuendelee kufanya kosa kwa kutengeneza serikali tatu?
“Kama ni kosa limefanyika, njia halali ni kusahihisha kosa. Kupokea na kulikubali kosa … kusema na sisi tuendelee kushika njia nyingine sio sahihi,” amesema Pengo akifafanua njia bora ya kusahihisha kosa hilo.
Alisema hayo jana, alipozungumza na waandishi wa habari, kufafanua tamko lililotolewa hivi karibuni na Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), kupendekeza mfumo wa Muungano wa serikali tatu.
Kwa mujibu wa Pengo, mapendekezo hayo ya Muungano wa serikali tatu ni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na si sahihi kuyachukua na kuyaita ni msimamo wa Kanisa Katoliki.
“Kanisa Katoliki wakitaka kutoa msimamo wa Kanisa halitegemei tume au kikundi chochote. Baada ya Baraza la Maaskofu hukaa pamoja hasa kunapokuwa na kitu kikubwa na nyeti kama hiki, linamkabidhi mamlaka Mweyekiti wake, yeye ndiye anayeweza kuongelea msimamo, ambao unakuwa ni msimamo wa Kanisa,” alifafanua.
Pengo alianza kwa kuweka wazi kuwa yeye msimamo wake ni muundo wa Muungano wa serikali mbili na kufafanua kuwa huo ni msimamo wake binafsi na si kama Kadinali, au Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Alisema suala la Zanzibar kuwa na Katiba yao ni jambo ambalo lilipaswa kushughulikiwa na Serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar kwa kuhakikisha wanaondoa viashiria, vinavyoweza kuvunja umoja kwa kuzingatia Katiba iliyokuwapo wakati huo. “Vilipaswa kuangalia tangu mwanzo na Serikali ya Muungano na vile vile Serikali ya Zanzibar, hatuwezi kusema kwamba kwa kunyamazia jambo hilo wamefanya lililojema,” alisema.
Makosa na viashiria hivyo, yalitamkwa na  Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kuwa kuna vipengele katika Katiba ya Zanzibar,  vilivyosababisha wakubaliane na muundo wa serikali tatu, ikiwemo kipengele kinachotamka Zanzibar ni nchi.
Katika hoja ya Jaji Warioba, aliyoitoa katika mkutano wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) hivi karibuni, alisema baada ya kuchambua maoni ya wananchi, waliona kuwa ili kuwepo muundo wa Muungano wa serikali mbili, ni lazima kuwe na mamlaka kamili ya kusimamia sehemu zote mbili, kuwe na nchi moja na kuondoa mgongano wa kikatiba.
“Kwa kuondoa mgongano wa kikatiba, ina maana ni lazima Katiba ya Zanzibar isitamke kuwa ni nchi yenye mamlaka kama ilivyo sasa,” alisema Jaji Warioba.
Naye Msomi wa Taasisi ya Utafiti ya Umoja wa Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki na Kusini (ESAURP), Profesa Bonaventura Rutinwa wa Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),  alisema yapo makosa katika Katiba ya Zanzibar na Rasimu ya Pili ya Katiba mpya.
Katika Rasimu ya Pili, alisema kosa ni rasimu hiyo kutojipa nafasi ya kuwa Katiba Kuu, kuliko Katiba ya Zanzibar na itakayokuwa Katiba ya Tanganyika kwa mujibu wa mapendekezo ya Tume.
“Sasa kwa kuwa Zanzibar tayari ina Katiba yake, inayotoa na kulinda haki za kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa Wazanzibari, huhitaji nguvu za kinabii kubashiri kuwa Katiba ya Tanganyika ikija, itatoa na kulinda haki za kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa Watanganyika.
“Hii ikitokea, itasababisha wananchi kutoka Tanganyika wanaoishi Zanzibar na Wazanzibari wanaoishi Tanganyika kushindwa kudai haki zao za uraia kisheria,” alionya Profesa Rutinwa.
Alihitimisha kuwa katika mazingira hayo, mfumo unaopendekezwa wa serikali tatu, utafifisha mshikamano wa Watanzania na serikali za nchi washirika, na katika hali mbaya zaidi utazalisha kero mpya za Muungano zitakazokuwa na nguvu ya kuvunja Muungano.
Wakati Pengo akifafanua kuwa Katiba ya Zanzibar ina viashiria vinavyoondoa umoja wa kitaifa, na kuwa kuwepo kwa kosa hilo hakumaanishi kosa liendelezwe kwa kuunda serikali tatu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano, imefafanua kuwa baada ya kupatikana kwa Katiba mpya, Katiba ya Zanzibar itafanyiwa marekebisho.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, anayeshughulikia Muungano, Samia Suluhu Hassan, alisema hayo alipokutana na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, kuzungumzia  mafanikio na changamoto za Muungano, uliofikia miaka 50 sasa.
Marekebisho hayo kwa mujibu wa Samia, yataanzia katika suala la umiliki wa ardhi Zanzibar,  katika  kipengele cha Katiba ya Zanzibar kinachotoa haki ya kumiliki ardhi kwa Wazanzibari pekee.
“Tumeshakubaliana pande mbili za Zanzibar na Tanzania Bara katika kutatua kero za Muungano kuwakipengele hicho kiondoshwe au kurekebishwa na kusomeka kuwa ardhi ni mali ya Watanzania wote,” alisema.
Marekebisho hayo, Samia alisema yatatoa fursa kwa Watanzania kutoka Tanzania Bara, kumiliki ardhi Zanzibar na kumaliza malalamiko ya miaka mingi ya   kunyimwa fursa ya kumiliki ardhi Zanzibar.
Marekebisho mengine yatafanyika katika vikosi vya ulinzi vilivyopo Zanzibar, ambavyo vinateuliwa na Rais wa Zanzibar ambapo Samia alisema kipengele hicho cha Katiba ya Zanzibar, kitarekebishwa ili kuondoa ukinzani wa sasa unaosema vikosi vya ulinzi vinasimamiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano.
“Hii inaonekana kukinzana na litafanyiwa marekebisho baada  ya kukamilisha Katiba ya Jamhuri ya Muunganoingawa kiundani ukiangalia vikosi anavyounda Rais wa Zanzibar si vya ulinzi na usalama bali ni vya kutoa huduma na hata Katiba ya Zanzibar inavitambua kamaidara maalum lakini watu hawaelewi,” alisema.
Alitaja changamoto nyingine katika kutatua kero za Muungano kuwa ni ukosefu wa rasilimali fedha katika kutekeleza yanayokubaliwa na kamati ya pamoja ya Muungano.
Pia changamoto nyingine ni sheria zinazokinzana ambapo uamuzi unapofikiwa na wanasiasa huchukua muda mrefu kwa watendaji kutekeleza.
Alitaja mafanikio ya miaka 50 ya Muungano kuwa ni pamoja na kupatikana kwa ajira kwa pande zote mbili ambapo Watanzania kutoka Zanzibar wamewekeza kibiashara na kwenye kilimo Tanzania Bara na kutoka Bara wamewekeza sehemu mbalimbali Zanzibar kama kwenye ujenzi wa hoteli za kitalii.
“Vyakula vya Zanzibar kama mboga na viazi kwa asilimia 80 vinatoka Tanzania Bara, vyama vya siasa vilivyopo ni vya kitaifa vipo pande zote za Muungano navinawakutanisha wote kwenye Bunge na uchaguzi,” alisema.
Mafanikio mengine ni Watanzania kuwa na uhuru wa kuzungumza watakalo, kuwepo utulivu, amani na usalama na kusaidiana katika majanga.
Kuhusu taarifa kwamba TEC imetoa msimamo kutaka muundo wa serikali tatu na kwamba utapelekwa bungeni, Pengo alisema haiwezekani na si sahihi kuchukua maoni ya Tume na kueleza kuwa ndio maoni na msimamo wa Kanisa Katoliki.
Alisema kanisa haliwezi kutoa msimamo ambao waumini wanatakiwa kuufuata kuhusu serikali tatu, bali hutoa maoni katika masuala yanayogusa imani na maadili.
“Maoni ya Tume hayawezi kufanywa kuwa maoni ya Kanisa. Nasisitiza hili kwa sababu Kanisa linapotaka kutoa tamko ambalo waumini wake ni lazima walishike, ni pale linapogusa imani au maadili hapo ndipo Kanisa lina uwezo kamilifu wa kutamka kitu ambacho ni tamko la kanisa.
“Mfano, kungetokea pendekezo linalosema Katiba yetu itasema hakuna Mungu, Kanisa lingepaswa kusimama na kulisemea kuwa hatuwezi kukubaliana nayo kwa sababu inakwenda kinyume na msingi wa imani yetu, sisi tunaamini kwamba yuko Mungu na kukubaliana na wazo kwamba Mungu hayupo ingekuwa ni kukana imani yetu ya kidini.
Alitoa mfano: “Mimi ni mmoja wa viongozi katika Kanisa Katoliki nchini Tanzania, kama mapendekezo haya yanachukuliwa kuwa ni mapendekezo ya Kanisa Katoliki mimi ninayependelea serikali mbili je, ninafukuzwa katika kundi la viongozi wa Kanisa?
Utanitoa kwa haki ipi. Ningekuwa nimesema ndio kwa suala la kutoa mimba   hapo natakiwa kuondoka na huhitaji kuniondoa.”

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4510

Trending Articles