Image may be NSFW. Clik here to view. ![]() |
Ridhiwani Kikwete. |
Ridhiwani alishinda katika uchaguzi wa kura za maoni kumpata mgombea wa CCM katika uchaguzi huo uliofanyika jana katika jimbo hilo.
Mjumbe huyo aliibuka mshindi baada kupata kura 758, kati ya kura 1,316 zilizopigwa na kumwacha kwa mbali mgombea aliyemfuatia kwa kura, Iman Madega, aliyepata kura 335.
Mbali na Madega, ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, mwingine aliyegombea katika uchaguzi huo, ni aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Ramadhan Maneno, aliyepata kura 206.
Maneno, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, aliangushwa kwenye kura za maoni mwaka 2010 na aliyekuwa Mbunge katika jimbo hilo, Said Bwanamdogo, aliyefariki dunia Januari, mwaka huu na kuacha wazi nafasi hiyo.
Mgombea mwingine, Changwa Mohamed, ambaye alikuwa mwanamke pekee katika kinyang’anyiro hicho, aliambulia kura 12.
Hata hivyo, matokeo hayo na majina ya wagombea yatawasilishwa kwenye vikao vya juu vya CCM kwa ajili ya hatua zingine za utekelezaji kabla ya kutangazwa kwa mgombea.
Uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Chalinze umepangwa kufanyika Aprili 6, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Machi 12, mwaka huu, vyama vitawasilisha majina ya wagombea wake kwa ajili ya kuthibitishwa uteuzi wao. Machi 13, mwaka huu, vyama vitaanza kampeni zake kunadi sera kwa wapigakura na baadaye kusubiri siku ya uchaguzi.