Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4500

POSHO YAGAWA WAJUMBE BUNGE LA KATIBA, BAADHI WAKATAA NYONGEZA...

$
0
0
Wajumbe Bunge la Katiba.
Wakati Bunge Maalumu la Katiba likiunda kamati maalumu ya kufuatilia suala la nyongeza ya posho za wajumbe, umetokea mgawanyiko miongoni mwa wabunge hao.
Kamati iliyoundwa itafuatilia na kisha kuishauri Serikali iwaongeze posho wajumbe hao huku baadhi yao, wakipinga na  kutaka wananchi wasimame kidete kuipinga.
Wakati Zitto Kabwe akiomba Rais Jakaya Kikwete kutoridhia ombi hilo la nyongeza ya posho na yeye kuahidi kutoipokea, Mbunge Mohamed Kessy amesema posho hiyo si halali na wananchi wana haki kuandamana ili kuipinga.
Hata hivyo mbali na hao walioonesha msimamo wa kupinga ongezeko, asilimia kubwa ya wajumbe wengi,  waligeuka ‘mabubu’ huku wengine  wakitoa kauli za kubeza wanaokataa posho.
Kamati iliyoundwa jana na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge, Pandu Ameir Kificho, wajumbe wake ni Freeman Mbowe, Paul Kimiti,  Jenista Mhagama, Mohamed Aboud Mohamed na Asha Bakari Makame.
Mwingine ni William Lukuvi ambaye hata hivyo, baada ya jina lake kutajwa, asilimia kubwa ya wajumbe walizomea kuonesha kumkataa.
Ingawa haikufahamika sababu za wajumbe kutotaka awemo kwenye Kamati, Kificho alisema: “Timu hii pamoja na ambaye hamkumpigia makofi, tutafanya kazi pamoja hatimaye mtampigia makofi.”
Kificho alihakikishia wajumbe kwamba timu hiyo baada ya kukutana naye, pamoja na makatibu, itakuja na majibu mazuri. Alisema timu hiyo inayofanya kazi kama kamati ya uongozi, itashauri na hatimaye Serikali ione umuhimu wa kufanyia kazi suala la posho.
Baada ya taarifa hiyo kutolewa bungeni, Kessy ambaye ni Mbunge wa Nkasi Kaskazini, alisimama akitaka kuzungumza jambo lakini hakupewa nafasi.
Baadaye akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi, alishutumu hatua hiyo akisema ni unyonyaji kwa wananchi ambao wengi wanaishi maisha magumu.
Kessy ambaye alisomea waandishi ujumbe wa simu aliotumiwa na wananchi wa jimboni mwake, alieleza kushangaa  wabunge wanaodai kwamba Sh 300,000 hazitoshi wakati katika mikutano ya Bunge la kawaida, wanalipwa Sh 170,000 kwa siku ambazo zinatosha.
“Tumekuwa bungeni, nimekuwa mbunge, tunalipwa Sh 170,000 kwa siku. Kima cha chini Sh ngapi, walimu wanapata Sh ngapi kwa siku, wanaishi na wana wake na watoto … Bunge hili tulikuwa tukilipwa Sh ngapi? Nyie hamwonei huruma wananchi wenu!” Alisema Kessy kwa mshangao.
Alisema ingekuwa vizuri kama gharama za matumizi zingechanganuliwa kwa maana ya bei ya hoteli, chakula, usafiri ili wajumbe wavune jasho lao kwa kulipwa wanachostahili, kuliko kuumiza wananchi.
Miongoni mwa ujumbe wa simu alioonesha waandishi ulisema: “Wabunge ambao hawataki hiyo posho ya laki tatu (300,000/-) watoke warudi kwao.” Kessy aliunga mkono ujumbe huo akisema: “Wananchi wanalia kule hawana maji.”
Ujumbe mwingine ulisema: “Mbona huko bungeni wabunge hawatuombei nasi watumishi tupate Sh 700,000 kwa mwezi na wao ndio wanaoomba walipwe Sh 700,000 kwa siku, kweli Watanzania tuna haki kwa nchi yetu?”
Zitto alimwomba Rais Jakaya Kikwete asiidhinishe maombi hayo ya kuongezwa posho.  Alisema hata ikiongezwa, yeye hatachukua nyongeza.
Alisema hali ya maisha ya wananchi ni mbaya na akaonya wajumbe kutotumia fursa zao za ushawishi wa kisiasa kutaka kufaidika na Bunge hilo.
“Gharama za posho na nyongeza ambayo wabunge wanataka, katika hali halisi ya uchumi wa sasa na ukiangalia hali kima cha chini cha wananchi,  haielezeki,” alisema.
Aliendelea kusema: “Namshauri Rais asikubali kuongeza posho. Kiwango cha sasa kinatosha. Hatukuja humu ndani kujitajirisha wala kumaliza matatizo ya nyumbani. Hii si kazi ya kujitajirisha, hii si ajira.”
Alisema fursa hiyo ya kuwa sehemu ya mchakato huo,  inapaswa kila mjumbe ajivunie katika historia ya nchi kwa kushiriki kikamilifu badala ya kujielekeza kwenye posho.
“Ni jukumu lenu waandishi wa habari kufanya uchunguzi (wa gharama halisi za matumizi Dodoma ). Kuna wabunge wanakaa kwenye hoteli mnazokaa, kuna wabunge wanakula sehemu mnazokula, nyie mnalipwa Sh ngapi?” Alihoji Zitto.
Mchungaji Israel Natse alisema Katiba ni suala la kitaifa lenye maslahi kwa wananchi, ambalo hata wangeambiwa kufanya kazi bila malipo, ingewezekana kufanya.
“Hatuwezi kutanguliza masuala ya posho kabla ya kazi tuliyotumwa kufanya. Hata kama tungeambiwa tufanye bure tungefanya, kwa sababu ni suala la kitaifa,” alisema.
Natse ambaye ni Mbunge wa Karatu alisema Watanzania wanaishi maisha magumu. Alisema hata ikiangaliwa kiwango cha maisha kati ya wananchi na viongozi, lipo tabaka kubwa.
Wakati wengi wa wajumbe waliohojiwa na waandishi wa habari wakikataa kuzungumzia msimamo wao juu ya posho, wapo baadhi ambao walisikika wakibeza wanaopinga posho.
Wakati Kessy akizungumza na waandishi wa habari, mmoja wa wabunge maarufu, alisikika akibeza kwa kusema, “huyo hana hoja, mwulizeni hadhi ya hoteli anayolala,” akimaanisha kuwa Kessy hela yake inamtosha kwa kuwa anaishi kwenye nyumba ya kulala wageni wa hadhi ya chini. Hata hivyo, waandishi walipotaka Mbunge huyo, azungumze rasmi, alikataa.
Wakati baadhi ya wajumbe, akiwamo Richard Ndassa Mbunge wa Sumve, aliyeibua suala hilo la posho juzi, wakidai wana hadhi ambayo inawalazimu kuishi kwenye hoteli za gharama, mwandishi alibaini kuwapo wengi wao wanaoishi katika hoteli za kawaida mitaani.
Miongoni mwao wanaishi katika hoteli zinazoanzia Sh 15,000 hadi Sh 30,000 kwa siku ambazo hata hivyo huduma zao ni nzuri. Ufuatiliaji wa gazeti hili, umebaini chumba cha Sh 20,000 kina  televisheni, kitanda kikubwa, choo cha ndani huku asubuhi mhusika akipata kifungua kinywa.
Kwa wanaoamini katika hoteli za hadhi ya juu, uchunguzi wa mwandishi umebaini wengi wanalipia si zaidi ya Sh 70,000 katika hoteli za hadhi ya juu ingawa pia vipo vyumba vya zaidi ya Sh 100,000 katika hoteli hizo.
Kwa upande wa usafiri, wasio na magari binafsi, zipo teksi ambazo kwa usafiri ndani ya Dodoma kwa masafa mafupi, nauli ni wastani wa Sh 3,000 hadi Sh 7000 kwa  kuzingatia umbali  wa safari, lakini nyingi ya hoteli zipo katika usawa wa wastani wa Sh elfu tatu kwa maeneo ya kati ya mjini na Sh 7,000 pembeni kidogo.
Hivyo kwa siku inakadiriwa mjumbe anaweza kutumia si zaidi ya Sh 14,000 kwa usafiri kwa maana ya kwenda bungeni na kurudi kwenye makazi yake.
Kuhusu chakula, katika mgahawa wa bungeni, kifungua kinywa kinaweza kupatikana kuanzia Sh 1,500 na kuendelea kulingana na ulaji wa mtu. Kwa upande wa chakula, kinapatikana kuanzia Sh 5,000 kulingana na utashi wa mtu.
Vile vile mtaani, katika baadhi ya hoteli, zikiwamo ambazo nyingi wamefikia wajumbe, chakula kinapatikana kuanzia Sh 4,500 na kuendelea.
Mathalani, katika hoteli mojawapo iliyo jirani na Bunge, ambako wajumbe wengi wamefikia, mwandishi alipata mchanganuo kwamba bei ya chumba ni Sh 15,000, Sh 20,000 na Sh 30,000.
“Kitanda ni cha futi tano kwa sita, kuna televisheni, kifungua kinywa ni chai, mkate, juisi na mayai. Bei ya chakula ni kati ya Sh 5,000 na Sh 7,000 kulingana na unachoagizia,” alisema mhudumu wa hoteli hiyo.
Juzi bungeni, Ndassa alidai wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameongezwa posho na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar jambo ambalo linaleta tofauti bungeni.
Akiungwa mkono na Suleiman Nchambi ,  walihoji sababu za wao kupewa posho hiyo wakati wajumbe wa Tume ya Marekebisho ya Katiba walilipwa Sh 500,000 walipokuwa wakikusanya maoni ya Katiba.
Kwa mujibu wa wanaotaka nyongeza, mchanganuo wa matumizi yao ni kwamba hadhi ya hoteli wanayopaswa kulala ni ya kuanzia Sh 70,000. Pia wanahitaji  mafuta ya magari, kulipa madereva na kutoa fedha kwa watu  wanaowaomba msaada.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4500

Trending Articles