![]() |
Bernard Membe. |
Membe na makada wengine watano wa chama hicho, wanatuhumiwa kuanza kampeni mapema kinyume cha utaratibu na mwongozo wake.
Makada wengine, ni waliopata kuwa mawaziri wakuu, Frederick Sumaye na Edward Lowassa; Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wasira na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba.
Wote waliitwa Dodoma na kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Maadili kuhusu madai ya kuanza kampeni mapema zinazodaiwa kuivuruga CCM na wanachama wake nchini.
Juzi, baada ya kumalizika kuwahoji Jumapili iliyopita, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alitangaza Dar es Salaam adhabu hiyo.
Nape alisema baada ya kuwahoji, walithibitika kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea urais kabla ya wakati, jambo ambalo ni kinyume cha Kanuni za Uongozi na Maadili ya CCM.
Akizungumza jana bungeni Dodoma, Membe alisema leo atakuwa na la kuzungumza kuhusu adhabu hiyo.
“Kesho (leo) nitazungumza, nitakuwa na cha kusema,” alieleza na kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge akifuatana na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Wasira alipoulizwa msimamo wake, kwanza alisema hana cha kuzungumza kuhusu adhabu hiyo, lakini baadaye akasema: “Mahakama ikishatoa hukumu, huna budi kutii.
“Nimesikia yaliyotangazwa, sina cha kuongea,” alisema Wasira, lakini alipobanwa zaidi na waandishi akarudia kauli hiyo hiyo.
Ngeleja hakutaka kuzungumzia hilo, akisema hana maoni kuhusu uamuzi huo, huku Lowassa kupitia kwa mmoja wa wasaidizi wake, akisema pia hana cha kuzungumza.
Sumaye kama ilivyokuwa kwa Januari, hawakupatikana kuzungumzia hatua hiyo ambayo sasa itawafanya makada hao sita kukaa chonjo, vinginevyo wanaweza kutangazwa kukosa sifa ya kugombea uongozi kwa tiketi ya CCM.