![]() |
Spika wa muda, Pandu Ameir Kificho. |
Aidha, mjumbe huyo hatalipwa posho yoyote isipokuwa ya kujikimu ambayo ni Sh 80,000 kwa siku.
Hayo ni miongoni mwa mapendekezo ya Rasimu za Kanuni za Bunge Maalumu la Katiba, ambazo wajumbe wake zaidi ya 600 walianza kuzipitia jana na watazijadili kabla ya kuamua kuridhia kuwa Kanuni Rasmi za Bunge Maalumu la Katiba za Mwaka 2014.
Kanuni ya 94, inampa mamlaka maalumu Mwenyekiti kuhakikisha amani na utulivu bungeni.
Kanuni hizo zinasema iwapo hali hiyo itatokea kwa mjumbe, Mwenyekiti ataamuru Mpambe wa Bunge amtoe mara moja nje na asihudhurie vikao vya Bunge na kamati zake kwa siku kumi.
Kanuni ya 96, inapendekeza kuwa mjumbe aliyesimamishwa kuhudhuria vikao, atatoka bungeni na hataingia sehemu yoyote ya ukumbi wala maeneo ya Bunge.
“Pia hatahudhuria vikao vyovyote vya kamati za Bunge kwa muda wote atakapokuwa amesimamishwa na hatalipwa posho nyingine yoyote isipokuwa ya kujikimu,” inaeleza kanuni hiyo.
Aidha, endapo mjumbe aliyeadhibiwa ataomba radhi kwa makosa aliyofanya, Mwenyekiti anaweza amsamehe baada ya kuzingatia maoni ya wajumbe kupitia Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge.
Kanuni hizo pia zinaeleza kuwa ili kudhibiti fujo ikitokea ndani ya Bunge na Mwenyekiti kuona haja ya kutumia nguvu, ataahirisha shughuli bila hoja kutolewa au kusitisha kikao kwa muda atakaotaja.
Kutakuwa pia na adhabu ya kuonywa na Mwenyekiti, kutolewa nje kwa muda uliosalia wa kikao cha siku au kutohudhuria vikao vitatu kwa mjumbe atakayekaidi kufuta kauli za lugha za matusi, usafiri, uchokozi
au lugha ya matusi.
Rasimu hiyo inaeleza pia kuwa shughuli za Bunge zitaendeshwa kwa lugha ya Kiswahili na wajumbe watavaa mavazi nadhifu na ya heshima kwake na kwa Bunge, utamaduni wa nchi na yasiwe na alama au rangi inayoashiria chama cha siasa.
Inapendekeza pia kuwa vikao vitaanza saa tatu asubuhi hadi saa saba mchana na kurejea saa 10 jioni hadi saa 2 usiku.
“Mjumbe ambaye atashindwa kuhudhuria kikao cha Bunge hatalipwa posho ya kikao au vikao alivyoshindwa kuhudhuria,” ilieleza.
Rasimu inapendekeza mambo kadhaa yasiyoruhusiwa bungeni; baadhi yao ni kusema uongo, kutoa taarifa zisizokuwa na ukweli, kutumia jina la Rais kwa dhihaka au kwa madhumuni ya kutaka kushawishi Bunge liamue jambo kwa namna fulani.
Mengine ni kumsema vibaya au kutoa lugha ya matusi dhidi ya Mwenyekiti, Makamu, mjumbe au mtu mwingine yeyote, kutumia lugha ya kuudhi au inayodhalilisha watu wengine.
“Mjumbe yeyote anapokuwa akisema ndani ya Bunge hatachukuliwa kuwa anasema uongo iwapo atafanya rejea ya andiko la kitabu au utafiti kuhusu jambo fulani au habari kuhusu jambo hilo iliyotangazwa au kuandikwa na vyombo vya habari,” inaeleza Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalumu.
Kuhusu muda wa kuzungumza, inapendekezwa kila mjumbe anayejadili hoja, apewe muda usiozidi dakika 10.
Kutakuwa na vikao vya faragha, ambavyo hakuna mtu asiye mjumbe au mtumishi wa Bunge, atakayeruhusiwa kuhudhuria katika sehemu yoyote ya ukumbi.
Ila Mwenyekiti wa Bunge anaweza kutoa taarifa fupi kwa wananchi kupitia vyombo vya habari kuhusu majadiliano na uamuzi uliofanywa na Bunge katika kikao chake cha faragha, kama atakavyoona inafaa.
Rasimu hiyo inapendekeza kuwapo kamati 20 za Bunge la Katiba, ikiwamo Kamati ya Shughuli za Bunge Maalumu la Katiba na Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge Maalumu na Kamati ya Uandishi.
Aidha, kutakuwa na kamati namba moja hadi 17, ambazo pamoja na kazi zingine, zitakuwa na majukumu ya kujadili na kuwasilisha mbele ya Bunge taarifa kuhusu mambo yaliyo kwenye Rasimu ya Katiba kwa kuanzia na sura ya kwanza.
Watoro katika vikao vya kamati waatadhibiwa, kwani Rasimu inapendekeza asiyehudhuria vikao vitatu mfululizo bila taarifa, aonywe na Mwenyekiti wa Kamati, na kama ataendelea, atapelekwa kwa Mwenyekiti wa Bunge kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Kuhusu utaratibu wa kuwasilisha Rasimu ya Katiba, baada ya kuwasilishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mwenyekiti wa Bunge, atapeleka nakala za Rasimu ya Katiba katika Kamati ya Bunge Maalumu, na kila kamati itajadili Rasimu hiyo kwa mujibu wa mgawanyo wa majukumu yake.
Kuhusu mapendekezo ya marekebisho au mabadiliko yaliyokidhi matakwa na masharti ya kanuni, yatajadiliwa na kupigiwa kura kwanza, kabla ya sura au sehemu ya ibara inayohusika ya Rasimu ya Katiba kupigiwa kura na kupitishwa.
“Bila kuathiri masharti ya sheria na kanuni hizi, wakati wa uamuzi wa Bunge Maalumu kuhusu kupitisha Rasimu ya Katiba, Bunge litapiga kura ya siri, ambayo kwa madhumuni ya kanuni hii, itaitwa Kura ya Mwisho,” ilifafanua Rasimu ya Kanuni za Bunge.
Aidha, inapendekezwa kuwapo kwa kura ya siri au kura ya kieletroniki katika kufikia uamuzi.
Utaratibu baada ya kifo cha mjumbe wa Bunge hilo, unaopendekezwa ni kuahirisha shughuli za Bunge kwa siku hiyo kwa ajili ya maombolezo.
Kuhusu uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bunge, mjumbe anayetaka nafasi, atalazimika kujaza fomu maalumu na kulazimika kuungwa mkono na wajumbe wenzake 20 kutoka kila upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwiano wa 10:10.
Bunge Maalumu la Katiba lilianza kazi zake Jumanne na kuanzia Jumatatu litaanza rasmi vikao baada ya kuapishwa kwa Mwenyekiti na Makamu na kuzinduliwa na Rais Jakaya Kikwete.
Litadumu hadi Aprili 30, ingawa linaweza kuongezwa muda wa siku 20 kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.