![]() |
Zelothe Steven. |
Ajali hiyo ilitokea jana asubuhi eneo la Msijute nje kidogo ya Mtwara Mikindani, na kusababisha wanafunzi wengine 47 wa shule hiyo kujeruhiwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Zelothe Steven, alisema gari hilo aina ya Mercedes Benz, namba T 174 AED lilipamia wanafunzi hao kando ya barabara ya Mtwara Ð Lindi.
Alisema gari hilo lililokuwa likiendeshwa na Baraka Mgwegwe (50), lilipoteza mwelekeo na kugonga wanafunzi hao na kisha dereva kujisalimisha Polisi. Uchunguzi unaendelea kabla ya kumfikisha mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
Awali Kamanda Zelothe alisema ajali hiyo ilipoteza maisha ya wanafunzi wanne na 47 kujeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara ya Ligula, kwa matibabu na jitihada za madaktari zinaendelea ili kuokoa maisha ya majeruhi hao.
"Hadi sasa taarifa tulizonazo ni wanafunzi wanne ndio waliopoteza maisha na hali ya mmoja ni mbaya na madaktari wanaendelea na jitihada za kuokoa maisha yake tumwombe Mungu idadi hii isiongezeke," alisema Kamanda.
Lakini taarifa zilizopatikana baadaye zilieleza kuwa majeruhi mwingine ambaye alikuwa katika hali mbaya, alifariki dunia alasiri na kufanya idadi kuwa watano.
Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Saidi Mnyachi, alithibitisha kupokea majeruhi 47, huku 26 kati yao wakitibiwa na kuruhusiwa na wengine 21, wakiwamo wasichana 15 na wavulana sita, wakilazwa na wanaendelea na matibabu.
Dk Mnyachi alitaja waliopoteza maisha na kutambuliwa, kuwa ni Hailati Saidi, Mwanahamisi Mohamed, Nasma Salum na Idda Nguli, ambao miili yao imehifadhiwa katika hospitali hiyo huku utaratibu wa ndugu na jamaa kuwachukua kwa maziko ukiendelea.
Baada ya taarifa hiyo wakazi wa Mtwara Mikindani na vitongoji vyake walifurika katika hospitali hiyo kujua hatima ya watoto wao wa shule hiyo ya bweni yenye wanafunzi wa mikoa ya Lindi na Mtwara.
Shule hiyo ilijengwa na mfanyabiashara maarufu Mustafa Sabodo miaka minne iliyopita.