![]() |
Kabwe Zitto akisisitiza jambo katika mkutano na waandishi juzi. Kushoto ni Dk. Kitilla Mkumbo. |
Akizungumza na mwandishi kwa simu jana, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Dk Benson Bana, alibainisha kuwa kitendo cha Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitilla Mkumbo kujitokeza hadharani baada ya kuvuliwa madaraka kimeonesha ukomavu wao kisiasa.
"Haya yanayoendelea ndani ya chama hiki yanaonesha ni chuki na ubinafsi wa madaraka, yote haya tunayoyaona leo Chadema hayajielekezi kwenye sera na taratibu za chama hicho, kilizojiwekea," alisema Dk Bana.
Alisema chama hicho kwa muda mrefu kimekuwa kikituhumiwa kuwa na tatizo la ukanda na ufamilia, hivyo kilitakiwa kuondoa kwanza tuhuma hizo badala ya kuzizidisha kwa kuwavua viongozi wake uongozi haraka hivyo.
"Kwa mtazamo wangu, kiukweli uamuzi wa chama hicho dhidi ya Zitto na Dk Kitilla ulitolewa wakati ambao haukustahili na tuhuma zote zilizotolewa ni mambo ambayo yangeweza kushughulikiwa na kudhibitiwa na vikao vya ndani," alisema.
Dk Bana alisema kilichotokea kwa chama hicho kimezua maswali mengi miongoni mwa Watanzania na kuhoji uhalali wake, huku wengine wakiona chama hicho sasa kinabana fursa ya watu kuhoji au kutoa mawazo yao ndani ya chama.
"Sisi wana demokrasia tunaona adhabu iliyotolewa ni kubwa kuliko tuhuma, inabidi chama hiki kijipange na kuendeshwa kwa misingi kiliyojiwekea ili kiwe cha wote, vinginevyo wananchi watakuwa na wasiwasi nacho hasa katika eneo la kukabidhiwa Dola," alisema.
Kuhusu waraka unaodaiwa kutaka kuleta mabadiliko ndani ya chama hicho, uliondaliwa na Dk Kitilla na wenzake, Dk Bana aliusifu na kubainisha kuwa haukuwa na ubaya wowote na kamwe hauwezi kuchukuliwa kama uhaini.
Alisema kitendo cha wanachama wa chama hicho kufikiria kuandaa waraka kama huo kwa lengo la kutaka mabadiliko ni cha kawaida kwa vyama vingi vya siasa duniani, huku akitolea mfano kuwa hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipata kuandika kitabu chenye dhima kama hiyo.
"Nawapongeza walioamua kuandaa waraka huo, kwani si mara ya kwanza kwa watu kufanya hivyo ndani ya chama, hata Nyerere aliandika kitabu cha 'Uongozi na Hatma ya Nchi Yetu', baada ya kuona Serikali inafanya madudu, kitabu hicho kililenga kuwapa fursa viongozi wajikosoe," alisema.
Alishauri viongozi wa Chadema kutodharau waraka huo na badala yake wausome kwa kina na kufanyia kazi udhaifu uliobainishwa dhidi yao na kujirekebisha.
Mhadhiri Mwandamizi wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari, Dk Ayoub Rioba, alisema anauchukulia mgogoro wa Chadema kama matumizi bora ya demokrasia.
"Hii inaonesha hawa ni watu wanaotofautiana na si wanaoafikiana kila kitu, lakini pia nimeguswa na namna Zitto na Kitilla walivyochukulia mgogoro mzima na kwa kweli wameonesha ukomavu," alisema Rioba.
Alisema angesikitika na kuogopa iwapo angesikia kuwa viongozi wa chama hicho wanakubaliana kila kitu, ingawa alionya kuwa si kwa Chadema pekee, bali kwa vyama vyote vya siasa nchini kuhakikisha kuwa vinafuata misingi viliyojiwekea ya kuhakikisha nidhamu ndani ya chama.
Zitto, na Dk Kitila na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba walivuliwa uongozi wao kwa madai ya kuhujumu chama hicho.
Hata hivyo, juzi Zitto na Dk Kitilya walijitokeza hadharani na kubainisha misimamo yao, ikiwamo kutong'oka ndani ya chama hicho na wataendelea kuwa waaminifu na kufuata misingi yote ya chama hicho.
Wakati huo huo, uongozi wa Chadema leo utatoa ufafanuzi dhidi ya kauli inazodai kuwa ni za uongo na upotoshaji zilizotolewa na viongozi waliosimamishwa uongozi na Kamati Kuu ya chama hicho.
Akizungumza jana kwa njia ya simu, Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene alisema pamoja na suala hilo, lakini pia chama kitatoa tamko na uamuzi wa Kamati Kuu kuhusu hali ya siasa nchini.
Alisema uamuzi huo utaangalia zaidi maisha ya Watanzania ikiwa ni hatua ya kukamilisha mkutano wa Kamati hiyo uliofanyika mwishoni mwa wiki.
Katika kauli yake juzi, Zitto alisisitiza kwamba hatotoka katika chama hicho, huku akitoa ishara kwamba 'atamkabili' Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe, katika uchaguzi mkuu wa chama hicho mwakani.
Aidha, katika mkutano huo na waandishi wa habari, Mkumbo, alimsafisha Zitto, akidai hakuhusika na mkakati wa kuung'oa uongozi ulioko madarakani wa Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa.
Kadhalika Mwanasheria wa wanasiasa hao, Diwani wa Mabogini Moshi Vijijini, Albert Msando (Chadema), ambaye alipata pia kuwa Mwanasheria wa Mbowe katika kesi zake Arusha, alielezea kumkabili Mwanasheria Mkuu wa Chama hicho, Tundu Lissu, kwa madai ya kukiuka Katiba ya chama, wakati wa kutangaza kumvua Zitto madaraka yote ndani ya chama.
Kuhusu usafi wa Zitto, Dk Mkumbo alikiri kwamba yeye ndiye aliyeandaa na kuhariri waraka wa mkakati wa kuung'oa madarakani uongozi wa sasa wa juu wa Chadema, akishirikiana na Mwigamba na kiongozi aliye na nafasi za juu katika chama hicho, ambaye alisema muda ukifika atajitaja mwenyewe.