![]() |
Marehemu Jerry Mruma. |
Jerry aliyekuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Marekani (USIU) tawi la Nairobi, aliuawa nchini humo mwishoni mwa wiki iliyopita na anatarajiwa kuzikwa leo katika makaburi ya Kinondoni.
Kabla ya maziko, ratiba ya mazishi inaonesha kuwa kutakuwa na ibada itakayofanyika saa 7.00 mchana katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Usharika wa Mbezi Beach, lililopo eneo la Tangi Bovu.
Baadhi ya ndugu jamaa na marafiki waliojitokeza kupokea mwili huo, walibubujikwa machozi wakati walipokuwa wakitoa pole kwa wazazi pamoja na wanafamilia wengine, akiwepo kaka wa marehemu Khan na mdogo wake Kelvin.
Marehemu ni mtoto wa aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa Tanzania Standard Newspapers (TSN), Isaac Mruma, ambaye sasa ni mwajiriwa wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Jerry mbali na kuwa mwanafunzi, pia alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Kilimo Yetu jijini Nairobi, inayojishughulisha na masuala ya kilimo.
Msiba huo uko nyumbani kwa Mruma katika eneo la Mbezi Beach karibu na ghorofa za Benki Kuu.
Mwili wa Jerry ambaye alikuwa akisoma Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Biashara (MBA), ulipatikana mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kijana huyo kuripotiwa wakati akitoka katika hafla ya Usiku wa Mtanzania.
Taarifa ya awali iliyotolewa na chuo hicho kuhusu kutoweka kwa Jerry tangu Jumamosi iliyopita, ilisema alikuwa akitafutwa, kabla ya mwili wake kukutwa baada ya msako ulioongozwa na Kaimu Mkuu wa Usalama wa Chuo, Polisi na wanajumuiya wa chuo hicho.