![]() |
Jeneza lenye mwili wa Dk Sengondo Mvungi baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam jana. |
Kwa mujibu wa taarifa ya Msemaji wa Tume hiyo, Omega Ngole, shughuli ya kuaga mwili huo itatanguliwa na ibada ya kumwombea itakayofanyika pia kwenye viwanja hivyo kwa dakika 45 kuanzia saa 4:00 asubuhi.
Aidha, baada ya salamu za rambirambi na neno la shukrani, mwili utaagwa rasmi kitaifa kuanzia saa 6.30 mchana na kisha utapelekwa nyumbani kwake Kibamba-Msakuzi.
Ratiba inaonesha kuwa, kesho Jumapili kutakuwa na ibada fupi nyumbani kwake na baada ya hapo, safari ya kuelekea kijijini kwake Chanjale, Kisangara Juu wilayani Mwanga, Kilimanjaro tayari kwa maziko yaliyopangwa kufanyika keshokutwa.
Dk Mvungi alifariki dunia, Jumanne iliyopita kwenye Hospitali ya Milpark Johannesburg, Afrika Kusini baada ya kuumizwa na watu wasiojulikana waliomvamia nyumbani kwake, usiku wa Novemba 2 mwaka huu.