![]() |
Ujenzi huo ukiendelea eneo la Ubungo kabla ya jana vibarua kuamua kugoma tena. |
Wakizungumzia suala hilo jana, baadhi ya wafanyakazi hao waliozuia lango la kuingilia katika ofisi za kampuni hiyo Ubungo kupinga uamuzi huo, walisema kitendo hicho ni ukiukwaji wa haki zao huku wakiomba kukutana na viongozi wa juu wa Serikali.
Walisema uongozi wa Strabag Jumamosi uliwapa taarifa za kusitisha mkataba wao na wafanyakazi hao na kuwaunganisha na LABA kwa ajili ya mkataba mpya uliopaswa kuanza utekelezaji wake juzi kwa malipo ya Sh 10,000 kwa siku kutoka Sh 170,000 walizokuwa wakilipwa na Strabag kwa siku.
"Tumefanywa kama wanyama, mtu anakuja ghafla na kukueleza kuwa kuanzia sasa mwajiri wako mtu fulani bila kufuata taratibu za kazi.
"Sisi tumefanya kazi na Strabag kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa lazima kuwe na haki zetu," alisema mmoja wa wafanyakazi hao ambaye hata hivyo hakupenda jina lake liandikwe.
Mwenyekiti Chama cha Wafanyakazi (TAMICO) tawi la Strabag, Abdullah Rukusa, alisema uamuzi uliochukuliwa na Strabag ni ubabe kwa wafanyakazi wao na kuongeza, kuwa hawakubaliani na hatua hiyo na kwamba tayari wametoa taarifa ngazi za juu.
Alisema hata alipofuatilia suala hilo kwa afisa mwajiri wa Strabag aliyemtaja kwa jina moja la Nelson, hakupewa majibu ya kuridhisha.
Mwandishi alipomtafuta ofisa mwajiri wa Strabag kwa njia ya simu ya mkononi ili kuzungumzia suala hilo hakupatikana kutokana na ya simu yake kuita bila kupokewa.
Mkurugenzi Mtendaji wa LABA, Emmanuel Mshana, alisema kampuni yake haina tatizo na kwamba imeingia mkataba wa mwaka mmoja na Strabag kusimamia vibarua huku akidai kushangazwa na mgomo wa vibarua hao.
Alisema kwa kuwa tayari wana mkataba na kampuni hiyo, kwa sasa wanasubiri uamuzi itakaofikiwa na wafanyakazi hao ili aendelee na majukumu yake ya kazi.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki alipioulizwa kuhusu suala hilo alisema: "Nimesikia kuhusu suala hilo lakini kwa sasa siwezi kuzungumzia chochote kwa kuwa sijaonana nao."