![]() |
Pikipiki maarufu kama 'Bodaboda' zikisubiria abiria. |
Kutokana na Tanzania kuwa eneo linalofaa kwa uwekezaji kwa sababu ya kuwa na mazingira rafiki, Serikali ya Japan imeiteua kuwa kitovu chake cha biashara na uwekezaji barani Afrika.
Lengo la hatua hiyo ya kuonesha kuibuka kwa ushirikiano mkubwa zaidi baina ya nchi hizo mbili, ni kuifanya Tanzania iimarike kiuchumi na hivyo kutengeneza ajira zaidi kwa watu wake.
Uamuzi huo wa Japan unatokana na mazungumzo kati ya Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe yaliyofanyika Tokyo, Japan, Rais Kikwete alipotembelea nchi hiyo Juni, mwaka huu.
Msimamo huo mpya wa Japan ulitangazwa rasmi jana na Waziri wa Uchumi, Biashara na Viwanda wa nchi hiyo, Toshimistu Motegi alipozungumza na Rais Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji na Uwezeshaji, Mary Nagu; Waziri wa Viwanda na Biashara , Dk Abdallah Kigoda na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe.
Waziri Motegi alimwambia Rais Kikwete kuwa ametumwa na Waziri Mkuu Abe kufuatilia mazungumzo yao na kutangaza rasmi kuwa Japan imeiteua Tanzania kuwa nchi lengwa na kitovu cha uwekezaji wa nchi hiyo katika Afrika Mashariki na Afrika yote.
Pia alimwambia Rais Kikwete kuwa yuko nchini kutoa taarifa kuwa Japan iko tayari kushiriki kuboresha na kuifanya kuwa ya kisasa zaidi Reli ya Kati kwa kujenga njia ya kimataifa badala ya nyembamba iliyopo sasa.
Aliongeza kuwa Japan itatuma wataalamu wake kuja nchini kuangalia jinsi ya kuanza kazi ya uboreshaji wa reli hiyo.
Aidha, Motegi alitangaza kuwa Japan itashiriki upanuzi na uboreshaji wa bandari ya Dar es Salaam kwa kuifanya nayo iwe ya kisasa zaidi.
Waziri Motegi alisema katika azma ya Japan kuifanya Tanzania kuwa nchi ya mfano katika Afrika kwenye uwekezaji na uchumi imara, anafuatana na kundi la wafanyabiashara ambao wanaendelea na mazungumzo na wafanyabiashara wa nchini ili kuona jinsi wanavyoweza kusaidiana kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.
Pia alisema moja ya malengo ya uamuzi huo ni kuhakikisha bidhaa ambazo kwa sasa zinanunuliwa moja kwa moja kutoka Japan, zinazalishwa nchini katika viwanda vitakavyojengwa na kampuni za nchi yake.
Kwa kuanzia, alisema kampuni mbili za Honda na Panasonic zimekubali kujenga viwanda nchini; kimoja kwa ajili ya pikipiki za Honda na kingine vifaa vya umeme.
"Huu ni mwanzo tu Mheshimiwa Rais, kwa sababu kama nilivyosema, tunataka Tanzania iwe nchi mfano ya uwekezaji wa Japan katika eneo hili la dunia na namna hiyo kwa pamoja tutakuwa tumeshirikiana kuongeza ajira kwa wananchi wa Tanzania," Motegi alimwambia Rais Kikwete.
Waziri huyo pia alisema baadhi ya kampuni za Japan zina mipango ya kuwekeza kwenye kilimo, hasa cha pamba na kujenga viwanda vya nguo nchini.
Wakati wa mazungumzo yao Tokyo, Japan, Rais Kikwete alimsihi Waziri Mkuu Abe, kuwekeza zaidi Afrika, akisisitiza kuwa Japan ni moja ya mataifa makubwa duniani ambayo yamepata soko kubwa Afrika na hasa la magari.
Uamuzi wa Japan na ziara ya Motegi inakuja miezi michache baada ya Tanzania kupokea viongozi wa mataifa mengi yakiwamo makubwa ya Marekani na China na inathibitisha ni kiasi gani siasa na sera za Tanzania zinavyokubalika duniani.
Wakati huo huo, Serikali ya Japan imekiri kuvutiwa na kuhamasishwa na fursa za uwekezaji zilizopo nchini hususan katika sekta ya nishati na imeonesha nia ya kuwekeza katika sekta hiyo pia.
Waziri Motegi alisema hayo hivi karibuni alipozungumza na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ofisini kwake Dar es Salaam.
Waziri Motegi, ambaye aliongoza ujumbe wa wafanyabiashara wa Japan, alitaja maeneo ambayo nchi yake ingependa kufanya uwekezaji kuwa ni pamoja na uzalishaji na usambazaji umeme.
Mbali na kuonesha nia ya kuwekeza nchini, Wajapani wameonesha utayari wa kusaidia Watanzania kusimamia na kuendeleza rasilimali zilizopo kwa kutoa mafunzo.
"Serikali yangu iko tayari kupokea wanafunzi wa Tanzania kwa mafunzo katika fani ya jotoardhi," alisema Waziri Motegi. Hata hivyo, alibainisha kuwa kwa sasa Serikali yake inafanya maandalizi ya kupokea Watanzania kwa mafunzo husika na endapo mambo yatakwenda sawa, mafunzo yataanza rasmi mapema mwakani.
Waziri Muhongo aliishukuru Japan kwa utayari wa kuwapa mafunzo Watanzania na kusisitiza kuwa hilo ni jambo la msingi kwa nchi kusimamia rasilimali zake kikamilifu.
"Serikali imedhamiria kuongeza wataalamu wazawa watakaosimamia rasilimali zetu vizuri bila kutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi," alisema.
Aidha, Profesa Muhongo aliwahakikishia Wajapani kuwa Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji na kuwakaribisha wafanyabiashara hao kuwekeza katika miradi ya uzalishaji na usambazaji umeme kupitia vipaumbele vilivyoainishwa na Serikali vya jotoardhi, tungamotaka, gesi asilia, upepo na umemejua.