![]() |
Madini ya Tanzanite. |
Mfanyabiashara maarufu wa madini jijini Arusha, Erasto Msuya amepigwa risasi na kufa papo hapo katika eneo jirani na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Msuya anayemiliki vitega uchumi kadhaa mkoani Arusha na Manyara, amepigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi wakati akitokea Mirerani katika migodi ya madini ya tanzanite, saa 6.30 mchana jana.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo kutoka uwanja wa ndege wa KIA ambao hawakuwa tayari kutajwa majina yao, mfanyabiashara huyo baada ya kuuawa hakuna kitu kilichochukuliwa katika gari yake.
"Hawa jamaa walimvizia njia ya panda ya Mirerani na KIA na walifanikiwa kumsimamisha na ghafla alitokea mtu akiwa katika usafiri wa pikipiki na kummiminia risasi nyingi na inaonekana alikufa papo hapo," alisema mtoa habari huyo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz hakupatikana kuelezea tukio hilo kutokana na simu yake kuita kwa muda mrefu bila majibu.