![]() |
Baadhi ya ombaomba wakiwa wamepiga kambi kando ya moja ya mitaa ya Dar es Salaam na watoto wao. |
Mkoa wa Dodoma unadaiwa kuongoza kwa kutoa idadi kubwa ya watoto wanaoomba mitaani katika Jiji la Dar es Salaam wakiwa na wazazi wao.
Katika utafiti uliofanywa mwaka huu na Shirika linashughulika na masuala ya Familia na Afya (FHI360) chini ya mradi wa Pamoja Tuwalee, kati ya watoto 332 waliohojiwa, asilimia 35.5 sawa na watoto 118, wamebainika wanatoka mkoani Dodoma.
Aidha kati ya watoto hao 332 wanaoomba, imebainika asilimia 13.6 wanatoka mkoani humo Dar es Salaam huku pia mkoa wa Mtwara ukishika nafasi ya tatu kutokana na kuwa na asilimia 3.3.
Mikoa mingine inatoa watoto kwenda jijini Dar es Salaam kuomba na asilimia kwenye mabano ni Singida (2.1), Lindi (1.5), Tanga (1.5), Kigoma (1.2), Mbeya (1), Ruvuma (0.6), Mwanza (0.3), Katavi (0.3) na Pwani yenye asilimia 0.3.
Akizungumza katika mkutano wa wadau uliojadili matokeo ya utafiti huo, ,Ofisa Mwandamizi wa shirika hilo, Judith Masasi alisema ongezeko la watoto wanaoomba tishio.
"Utafiti juu ya watoto hao ulifanywa na mradi wa pamoja tuwalee katika jiji la Dar es Salaam ambapo jumla ya watoto wanaozunguka wakiomba na wazazi wao 332 walihojiwa katika masuala mbalimbali,"alisema Judith.
Katika utafiti waliwahoji watoto hao kama wangekuwa tayari kurudi shule iwapo wangepewa nafasi ambapo inadaiwa asilimia 64 walisema wako tayari, asilimia 16 walisema hawataki na asilimia 20 hawakuwa na uamuzi kama wanahitaji huduma hiyo.
Alisema hata walezi ama wazazi wa watoto hao wapatao 151 ambao huzunguka na watoto walisema wazazi wao walikuwa ombaomba huku walezi wapatao 85 wakizaliwa na familia ambazo haijawahi kuwa ombaomba.
Akizungumzia suala la ombaomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Saidi Meck Sadiki katika hotuba yake iliyosomwa na Kaimu Mkuu wa mkoa,Viktoria Bura alisema ipo haja ya nguvu kubwa kuelekezwa kwa watoto wa aina hiyo ili kuwasaidia na kuokoa kizazi kijacho.