![]() |
Frederick Werema. |
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, ameagiza utaratibu wa zamani wa mawakili wa Serikali kupigiwa saluti, urejeshwe ili Dola iheshimiwe wakati wa kuendesha kesi.
Alisema hayo juzi katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa mjini hapa, katika mkutano wa mawakili wafawidhi wa Serikali, wakuu wa upelelezi wa mikoa na wakuu wa vikosi vya Polisi.
Aliagiza wakuu wa upelelezi wa mikoa na mawakili wafawidhi wa Serikali, kukaa kwenye meza moja na kujadili namna ya kurudisha utaratibu huo.
“Kufanya hivyo ni kuipigia saluti Serikali,” alisema Werema na kuongeza kuwa hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kulinda na kuheshimiwa kwa Dola, wakati wa kuendesha kesi mahakamani.
Alisema utaratibu huo ulikuwapo zamani, lakini ukaondolewa na aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Omari Mahita bila kufafanua sababu za kufanya hivyo.
Werema pia alikemea tabia ya mawakili wa Serikali na wapelelezi kushirikiana kufuta kesi baada ya kuhongwa na kuongeza kuwa tabia hiyo iko katika Dola za ovyo.
“Wakili wa Serikali anauza kesi, mpelelezi naye anauza kesi, hiyo ni Dola ya ovyo sana, hayo ni mambo ya ovyo ambayo yanatudhalilisha sana,” alisema.
Alisema Dola inatakiwa kuendeshwa kwa kalamu na si kwa maneno ya midomo, huku wajibu wa kutunza kumbukumbu kulingana na viapo ukizingatiwa.
“Kuna watu wananyofoa karatasi zenye maelezo ya mashahidi, wengine wanafanya kazi huku wanakunywa chai ambayo inaangukia kwenye majalada na kusababisha maandishi kufutika, tunza majalada usitafute ugomvi na sisi,” alisema.
Werema pia alikemea tabia ya baadhi ya askari Polisi kuonea wananchi kwa kuwabambikizia kesi ambazo hazina dhamana, zikiwemo za mauaji.
Alisema uonevu na upendeleo umesababisha malalamiko kutoka kwa wananchi kwa kuona kuwa hawatendewi haki kutokana na kubambikiziwa kesi za mauaji.
“Unamtafuta mtu lakini humpati kwa kosa lolote na wengine wanaamua kuwabambikizia watu kesi. Unamkamata mhalifu na kumwekea bangi mfukoni, si vizuri,” alisema.
Alitaka watendaji wanapofungua kesi mahakamani, kuarifu washitakiwa hasa ambao hawana mawakili na kuwe na mfumo rafiki wa kuwasiliana nao. “Msikamate mtu kama hakuna ushahidi wa kutosha.''
“Tunaposhuku mtu, tuwe na ushahidi basi, tusikamate watu siku ya Ijumaa ili tuwakomeshe wakae ndani mpaka Jumatatu ndio watoke,” alisema.
Alisema haki jinai inahusu haki na wajibu wa wapelelezi, waendesha mashitaka, watuhumiwa, walalamikaji, mashahidi na kumbukumbu za maelezo ya watuhumiwa.
Katika hatua nyingine, Werema alitaka majangili ambao kwa siku za karibuni wamekuwa wakiua tembo kwa kiwango cha kutisha, wadhibitiwe.
Aliomba Polisi kusaidia kudhibiti ujangili huo, kuhakikishia Watanzania wana uwezo wa kupambana na majangili na mawakili wasimamie vema kesi zinazopelekwa mahakamani, kwani tembo wengi wamekuwa wakipotea kwenye mbuga na hifadhi za Taifa.