Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4605

LWAKATARE AHUSISHWA SHAMBULIO LA MWANDISHI ABSALOM KIBANDA...

$
0
0
Wilfred Lwakatare.
Ofisa Mwandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare amekamatwa na Polisi na kuhojiwa kwa tuhuma ambazo hazijawekwa wazi.
Habari za kukamatwa kwa Lwakatare zilithibitishwa jana na Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, ambaye alisema hajui sababu za kukamatwa kwa Lwakatare ambaye ni Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama hicho.
"Taarifa za kukamatwa kwake ni kweli, lakini sababu ya kufanya hivyo waulizeni polisi wenyewe," alisema Makene ambaye hakutaka kuingia kwa undani juu ya suala hilo kwa maelezo kuwa alikuwa Kanda ya Ziwa kikazi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alipoulizwa habari za kukamatwa kwa Lwakatare, alisema "siwezi kukubali au kukanusha juu ya habari hizo, ila taarifa rasmi sijapata."
Kenyela alisema Dar es Salaam ina mikoa mitatu ya kipolisi, lakini pia kuna Kanda Maalumu ya Dar es Salaam pamoja na Makao Mkuu ya Polisi ambao mamlaka hizo zote zina mamlaka ya kufanya kazi sehemu yoyote ya Dar es Salaam.
"Tukio hilo linaweza kuwapo lakini sisi wa Kinondoni hatuhusiki na wala hatujapata taarifa yoyote," alisema kamanda huyo  ambaye ofisi ya makao makuu ya Chadema iko eneo lake la kazi.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, Suleiman Kova, alipotafutwa kwa njia ya simu, ilipokewa na msaidizi wake ambaye alisema bosi wake alikuwa kwenye kikao muhimu.
Licha ya kutokuwapo taarifa rasmi za kukamatwa kwa kiongozi huyo, lakini jana baadhi ya  mitandao ya kijamii ilionesha picha yake na kurusha sauti ikidaiwa ni ya kupanga mashambulizi dhidi ya baadhi ya waandishi wa habari na hivyo kuhusishwa kwa namna moja au nyingine na tukio la kushambuliwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda.
Hata hivyo, taarifa za ndani ya Jeshi la Polisi zilithibitisha kukamatwa kwa Lwakatare na kuhojiwa kwa saa kadhaa kuhusu picha hiyo na maudhui yake, ambapo pia alipekuliwa nyumbani kwake.
“Ni kweli Lwakatare alihojiwa hapa kuhusiana na picha zile zinazoonekana kwenye kompyuta ikiwa ni pamoja na sauti inayoelekeza kupanga mikakati ya kushambulia waandishi wa habari.
“Alihojiwa kuhusiana na hilo, lakini pia kubaini kama anaweza kuwa amehusika na shambulizi la Mhariri wa New Habari, Kibanda,” kilisema chanzo hicho cha habari ambacho hakikutaka kutajwa jina na kuongeza kuwa alipekuliwa pia nyumbani kwake.
Habari zilisema Lwakatare aliwasili makao makuu wa Polisi akiwa katika gari lake huku polisi nao wakiwa na gari lao, hali ambayo ilionekana hakukuwa na matumizi ya nguvu kumkamata kwani alitii bila shuruti.
Wakati akihojiwa alishuhudiwa na Wakili wake, Nyaronyo Kicheere ambapo pia alifuatana na ofisa wa kitengo chake cha Usalama aliyefahamika kwa jina la Hemed Sabula.
Katika video hiyo iliyoko kwenye mtandao wa Jamii Forum, Lwakatare anaonekana akitoa maelekezo kwa mtu ambaye atatimiza kitendo cha kumteka mtu, lakini kabla ya hapo afuatilie nyendo zake, ajue kama anamiliki silaha na kama anatumia pombe au hatumii.
Katika hatua nyingine, Kibanda ameanza mazoezi ya kusimama na kutembea ndani ya chumba alimolazwa katika hospitali ya Millpark, Johannesburg, Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena kwa vyombo vya habari jana, madaktari wanaomtibu wamesema amepata nafuu na kufanya hivyo kutamwezesha apate nguvu mwilini na kuujengea uwezo wa kujitegemea.
“Kwa jumla afya yake inaendelea kuimarika na madaktari pamoja na wauguzi wameendelea kumhudumia kwa karibu,” ilisema taarifa.
Walisema baada ya siku mbili au tatu kadri hali itakavyokuwa, wanatarajia kuanza mazoezi ya kumtembeza nje ya chumba katika jitihada hizohizo za kuuwezesha mwili kupata nguvu.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4605

Trending Articles