Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4503

TIBA ASILIA YAIACHA MIDOMO WAZI NIMR KATIKA UKIMWI...

$
0
0
Dk Julius Massaga akifafanua jambo.
Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Dawa za Binadamu (NIMR), imepokea dawa asili ambayo sasa inaonesha matumaini mazuri katika kukabiliana na virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Kuratibu Utafiti wa taasisi hiyo, Dk Julius Massaga, alisema NIMR inaifanyia utafiti wa kina dawa hiyo, kwa sababu imeonesha matumaini mazuri katika ugonjwa huo.
"Kuna waganga watatu walileta dawa zao kwa ajili ya utafiti wakidai zinatibu ugonjwa wa Ukimwi, moja ilikuwa katika hali ya unga lakini sasa tumeitengeneza katika vidonge na tunaendelea nayo na utafiti kwa kuwajaribu wagonjwa," alisema.
Waganga hao walikubali dawa zao kufanyiwa utafiti, baada ya kutengeneza mikataba nao, ndipo ikajulikana nguvu yake.
Dk Massaga alisema dawa hiyo inayodaiwa kutibu ugonjwa wa Ukimwi, ambao kwa miaka mingi sasa hauna tiba wala kinga, imeleta manufaa kidogo na hivyo watakwenda nayo mbali katika uchunguzi.
Hata hivyo, Dk Massaga alisema tiba asili imevamiwa na matapeli wengi, hasa katika miji mikubwa, ambapo waganga hudanganya watu kuwa wanatibu magonjwa mbalimbali, kumbe wanataka kujipatia fedha.
Nchi nyingi kama Asia kwa mujibu wa Dk Massaga, madaktari wa sayansi na wale wa jadi, hushirikiana katika matibabu kwa sababu huduma na dawa zao zimeboreshwa katika kiwango cha juu.
Mwaka huu, NIMR ina mpango wa kusajili dawa za jadi, jambo ambalo Dk Massaga alisema lilishindikana kwa sababu hawakuwa na mtambo wa uzalishaji wa dawa zenye ubora.
"Watu wanakosa imani na dawa za jadi kwa sababu hazina vipimo sahihi vinavyotambuliwa, lakini sasa tunaboresha na kuweka vipimo baada ya kuzifanyia utafiti dawa na kuwa na uhakika nazo," alisema Dk Massaga.
Alisema Serikali imejenga maabara na kiwanda cha kisasa cha daraja la kwanza, kwa ajili ya utafiti na utengenezaji wa tiba za asili katika eneo la Mabibo jijini Dar es Salaam, ambapo Sh milioni 800 katika mwaka huu wa fedha zimetengwa kwa ajili ya kumalizia ujenzi na kununua mitambo.
Changamoto nyingine katika kuaminiwa kwa dawa hizo, kuwa ni mitaala ya wataalamu wa tiba ya sasa, kutoelewa kwa kina juu ya tiba za asili, matumizi yake na vipimo vya tiba hizo.
Nyingine ni kutokuwepo kwa orodha ya miti yenye dawa, taarifa ya matumizi yake katika tiba, na muingiliano wa dawa za kisasa na za asili katika mfumo wa tiba.
Dk Massaga alisema taasisi hiyo imefanikiwa kutengeneza tiba asili zilizoboreshwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu, ikiwa ni pamoja na tiba za malaria, ini, magonjwa nyemelezi, kisukari, tezi dume, kikohozi na mafua, kuongeza nguvu za kiume na tiba ya maji ya kunywa.
Wakati huo huo, NIMR imesema iko katika utafiti kubaini kama mafuta ya ubuyu yana sumu au la, kama ilivyoelezwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).
TFDA katika taarifa ya hivi karibuni, iliwataka Watanzania kuacha kutumia mafuta ya ubuyu kwa kunywa, kwa kuwa yana tindikali ya mafuta, ambayo husababisha saratani za aina nyingi.
Mamlaka hiyo ilisema kuwa hawana tatizo na majani na unga wa ubuyu kutumika kwa kula, na hata mafuta hayo yakitumika kwa kupaka katika ngozi kama kipodozi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya TFDA, ili mafuta hayo yawe salama, lazima tindikali hiyo itolewe, lakini ikaonya kuwa Tanzania hakuna teknolojia ya kutenganisha tindikali hiyo na mafuta hayo.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4503

Trending Articles