![]() |
Miili ya askari hao ikiwa imewekwa tayari kusafirishwa kwenda mjini Khartoum. |
Miili ya wanajeshi saba waliouawa katika shambulio la kuvizia katika jimbo la Darfur nchini Sudan Jumamosi iliyopita, wanatarajiwa kurejeshwa nyumbani kwa maziko kati ya Alhamisi na Ijumaa.
Akizungumza na mwandishi kutoka katika kambi ya wanajeshi hao, Msemaji wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Darfur (UNAMID), Chris Cycmanick, alisema kwa sasa wanajiandaa kusafirisha miili hiyo hadi Khartoum, Sudan, kwa uchunguzi wa kitabibu.
"Marehemu wanne wamesafirishwa leo (jana), kwenda Khartoum kwa ajili ya uchunguzi na wengine watatu watasafirishwa kesho (leo).
"Tunatarajia uchunguzi utafanyika kwa siku moja au mbili na baada ya hapo watasafirishwa kwenda Tanzania. Nadhani kama ni kufika huko, itakuwa Alhamisi au Ijumaa," alisema Cycmanick.
Katika shambulio hilo kwa mujibu wa msemaji huyo, waliojeruhiwa walikuwa 17 na si 14 kama ilivyoelezwa mwanzo. Lakini Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), lilithibitisha, kwamba Watanzania waliojeruhiwa ni 14.
Cycmanick kwa upande wake, hakuwa na hakika na idadi ya Watanzania waliojeruhiwa ingawa alisema, kati yao Watanzania ndio wengi na kuna uwezekano wa askari wa mataifa mengine.
Pia alisema mpaka sasa hawana taarifa ya wahusika wa shambulio hilo na kazi inafanyika kujua wahusika na sababu za kushambulia msafara wa UNAMID.
Alipotakiwa kutaja hali ya majeruhi, Cycmanick alisema anajua kwamba wote wamelazwa hospitalini lakini hajui ni wangapi hali zao ni mbaya na wangapi wana nafuu.
Hata hivyo, Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe, alisema askari wanne Watanzania kati ya waliojeruhiwa, hali zao ni mbaya na wanapatiwa matibabu chini ya uangalizi maalumu wa madaktari katika eneo Hospitali ya Nyala.
Mgawe alisema taarifa zilizotolewa kwake na Ofisi ya Utawala ya JWTZ, wanajeshi hao wataendelea kuwa chini ya uangalizi maalumu wa madaktari, hadi afya zao zitakaporejea katika hali ya kawaida.
"Hadi sasa taarifa zilizoifikia ofisi yangu ni kuwa wanajeshi 10 kati ya 14 walikuwa wamejeruhiwa, wanaendelea vizuri na wanaweza kuwasiliana na wenzao wanaofika kuwaona pamoja na kutembea kutoka eneo moja hadi lingine, isipokuwa wanne hali zao si nzuri," alisema Kanali Mgawe.
Wanajeshi hao akiwamo askari wa usalama wa raia, walipatwa na mkasa huo wa kushambuliwa Jumapili wakati wakisindikiza msafara wa waangalizi wa amani walio nchini humo, wakati wakitokea kambi wanayoilinda ya Khor Abeche, kwenda kambi iliyopo Nyala.
"Wanajeshi wetu walipatwa na mkasa huo wakiwa katika utekelezaji wa jukumu lao la Umoja wa Mataifa la kulinda amani nchini Sudan eneo la Darfur," alisema Kanali Mgawe.
Kwa mujibu wa Cycmanick, wakati wakishambuliwa, msafara huo ambao ulikuwa ukilindwa nao, uligeuka na kujaribu kukimbia waasi.
Msemaji huyo wa UNAMID, alisema wakati wanakimbia shambulio hilo huku wakitoa taarifa, washambuliaji waliendelea kushambulia kwa silaha nzito.
Cycmanick alisema walituma askari wengine kutoka Nyala kwenda kuwasaidia lakini nao walishambuliwa, ingawa walifanikiwa kuokoa baadhi ya wenzao wakiwa majeruhi, na kwa bahati mbaya askari hao saba waliuawa.
Kuhusu maandalizi ya kupata ndugu wa marehemu hao, Kanali Mgawe alisema kila kitu kinashughulikiwa na Ofisi ya Utawala Makao Makuu ya JWTZ, na kuongeza kuwa ofisi yake itaendelea kutoa taarifa ya suala hilo kadri siku zinavyokwenda.
Alisema pia ujumbe uliotajwa kutumwa Sudani, taarifa zake zipo chini ya Ofisi ya Utawala huku akiahidi kuzitoa baada ya kufikishwa mezani kwake.
Tayari JWTZ imeweka bayana nia yake ya kuongeza nguvu ya kujilinda, wakati wa kulinda amani katika jimbo hilo, ili kujikinga na mashambulizi kama hilo.
Kanali Mgawe alisema mawasiliano yanafanyika kati JWTZ na UN, kuhusu uwezekano wa kuacha kutumia makubaliano ya UN Sura ya Sita, ambayo yanataka kusitumike nguvu sana.
Sasa Tanzania inapendekeza UN, iruhusu askari wake watumie Sura ya Saba, inayotoa fursa ya kutumia nguvu kujilinda, wanapokutana na tishio au shambulizi katika shughuli za kulinda amani.
Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya (EU), umeitaka Serikali ya Sudan kuchukua hatua za haraka kukamata watu waliohusika na shambulio dhidi ya askari hao, ili wafikishwe mbele ya sheria.
Taarifa ya EU iliyotolewa jana, ilimkariri Mwakilishi wake wa Mambo ya Nje na Sera za Usalama, Catherine Ashton, akilaani shambulio hilo lililosababisha vifo vya askari saba na majeruhi 17.
Ashton alituma salamu za rambirambi kwa Serikali, familia za askari hao pamoja na askari wote.
Akielezea kuguswa na hali tete ya usalama Darfur, Ashton alisema shambulio hilo, ni la tatu katika wiki tatu na kusema panahitajika nguvu za pamoja kuimarisha amani jimboni humo na Sudan kwa jumla.
Alisema EU inaunga mkono juhudi za pamoja za wawakilishi wa Umoja wa Afrika (AU) na UN walioko Darfur kulinda amani.