![]() |
Nape Nnauye. |
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshinda katika kata 16 kati ya 22 kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika nchini juzi.
Uchaguzi huo ni wa kujaza nafasi wazi za udiwani ingawa katika kata nne za Arusha, haukufanyika kutokana na mlipuko wa bomu kwenye mkutano wa Chadema uliosababisha vifo vya watu watatu na wengine wapatao 60 kujeruhiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa CCM Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema matokeo yaliyopatikana kutoka maeneo uchaguzi ulikofanyika yanaonesha CCM kwa asilimia 72.7 huku Chadema ikishinda kata sita sawa na asilimia 27.28
Alitaja kata ambazo CCM imeshinda na wilaya na mikoa yake kwenye mabano kuwa ni Stesheni (Nachingwea, Lindi), Genge na Tingeni ( Muheza, Tanga), Ubugile, Bahi na Dalai (Chemba, Dodoma) na Kata ya Langiro (Mbinga, Ruvuma) ambayo mgombea wa CCM alipita bila kupingwa.
Kata nyingine ni Manchila (Serengeti, Mara), Mbalamaziwa (Mufindi) na Ng’ang’awe (Kilolo, Iringa), Runzewe Magharibi (Bukombe, Geita), Mianzini (Temeke, Dar es Salaam), Minepa (Ulanga) na Masanze (Kilosa,Morogoro).
Kata nyingine ambazo CCM imeshinda ni Mkuyuni, (Monduli, Arusha) na kata ya Mnina, Mtwara.
Nnauye alizitaja kata ambazo Chadema imeshinda kuwa ni Nyampulukano (Sengerema, Mwanza), Iyela (Mbeya Mjini), Ifakara (Kilombero, Morogoro), Bashinet (Babati, Manyara), Dongobesh (Mbulu, Manyara)na Iseke, Singida.
Alishukuru wananchi walioonesha imani kubwa kwa CCM kwa kuipa dhamana ya kuendelea kuwatumikia.
“CCM inaahidi utumishi uliotukuka hata wale asilimia 27.28 walioamua kujaribu wenzetu tunawatakia kila la kheri, kwani wametumia haki yao ya kidemokrasia kuchagua wanaodhani watawasaidia kufikia malengo yao kimaendeleo,” alisema na kuongeza kuwa uchaguzi katika kata hizo umekwisha sasa kazi iliyobaki ni kutumikia wananchi.