Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4617

BOMU LALIPUKA MKUTANO WA CHADEMA NA KUACHA SABA MAHUTUTI ARUSHA...

$
0
0
Baadhi ya majeruhi wa mlipuko kwenye mkutano wa Chadema, Arusha jana.
Mwezi mmoja baada ya kutokea mlipuko katika Kanisa Katoliki la Joseph Mfanyakazi la Olasiti mjini hapa mlipuko mwingine umetokea katika mkutano wa kampeni wa Chadema na kujeruhi watu kadhaa.
Habari kutoka eneo la tukio zimedai kwamba mlipuko huo ulitokea karibu na gari la matangazo la Chadema aina ya Mitsubishi Fusso lililokuwa jirani na jukwaa alilokuwa akilitumia Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe jana jioni.
Taarifa zisizo rasmi zilidai kuwa watu saba wakiwamo watoto watatu walijeruhiwa vibaya na mlipuko huo na kukimbizwa katika hospitali ya Selian lakini hakuna kiongozi wa Chadema aliyejeruhiwa.
Hata hivyo habari zaidi zilisema viongozi wa Chadema, Mbowe, Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema na wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari walizingirwa na Polisi kwa ajili ya kuwapa ulinzi na kisha kuwaachia.
“Watu waliohudhuria mkutano huo katika uwanja wa Soweto katika kata ya Kaloleni walitawanyika baada ya mlipuko huo na kuchanganyikiwa zikiwa ni takriban siku 40 baada ya mlipuko wa kanisani ambapo watu watatu walipoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa.
Jana Chadema ilikuwa ikifunga kampeni zake eneo hilo kusubiri uchaguzi mdogo wa udiwani ambazo zinafanyika sehemu mbalimbali nchini sambamba na uchaguzi mdogo wa ubunge Chambani, Pemba, Zanzibar.
Sambamba na Chadema pia vyama vya CUF na CCM vilifunga kampeni katika eneo hilo moja, wakati CUF iliyohutubiwa na Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba ikifanyia stendi ya mabasi ya Kampala Coach, huku CCM ikihutubiwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye ilifunga kampeni zake katika kituo cha mabasi yaendayo Sanawari.
Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas azungumzire tukio hilo, hazikuzaa matunda kutokana na simu yake kuita bila kupokewa.
Mei 5 takriban watu watatu walikufa katika Kanisa hilo nje kidogo ya mji wa Arusha, na wengine kadhaa walijeruhiwa huku Balozi wa Vatican nchini na watawa waliokuwa katika shughuli maalumu ya kuzindua Parokia mpya ya Mtakatifu Yosefu walinusurika.
Wakati hayo yakitokea Arusha, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi amesema mantiki ya demokrasia ya vyama vingi si kujenga chuki, uhasama na ugomvi bali ni shime ya ushindani wa nguvu ya hoja itokanayo na ushawishi wa kisera bila umwagaji damu na mfarakano.
Alhaji Mwinyi alitoa kauli hiyo jana,  wakati akifunga kampeni za CCM katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mapape, mkoa wa Kusini Pemba.
Alisema mwanasiasa, mtu au mgombea wa nafasi ya uwakilishi anayetamani kutumia mfumo huo kinyume na upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa ni lazima jamii ianze kumwepuka.
“Hatukuruhusu demokrasia ya vyama vingi ili watu wahasimiane, wamwage damu au kutokee utengano wa kijamii, shindaneni kwa nguvu ya hoja na ulinganifu wa sera za vyama vya siasa,” alisema Mwinyi.
Aliasa wananchi wa Chambani kutojiingiza katika kadhia ya vurugu na mivutano inayoweza kuhatarisha maisha ya watu, hivyo aliwataka washiriki uchaguzi huo katika mazingira ya utulivu na amani bila rabsha.
Akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano huo,  Mwinyi alisisitiza kuwa wakati wa uongozi wake mwaka 1992 mfumo wa vyama vingi ulianzishwa na haukukusudia mvurugano, uhasama na chuki, bali Serikali yake ilitaka ushindani wa sera za vyama na jamii ikibaki bila ya mgawanyiko.
Rais mstaafu alisema dhana ya demokrasia ya vyama vingi isipotoshwe na wanasiasa ili kuigeuza nchi uwanja wa mapigano, vita na machafuko, na badala yake kila chama cha siasa kitambue kina wajibu na ulazima wa kuheshimu sheria za nchi na za kimataifa.
Akizungumzia mchakato wa uundwaji wa Katiba mpya, alisema dhana ya jambo hilo ina azma njema ya kuweka maagano ya pamoja ya kimfumo, kisheria na makubaliano yatakayohusisha uendeshaji wa nchi na watu wake, hivyo kila mtu atumie nafasi yake kutoa mawazo.
Alisema si haki kutokea kundi moja kuzungumzia lingine na  badala yake kila mwananchi apate fursa ya kutoa mawazo na kushauri namna bora ya kuongoza Taifa kwa msingi ya usawa, haki, demokaria na mpangilio wenye mwelekeo wa kuwa na uongozi bora, uwajibikaji, utii na nidhamu.
Akimnadi mgombea wa CCM Chambani, Mattar Sarahan Said, alitaka wananchi kumchagua mgombea huyo kwa kuwa anatokana na chama kinachofuata miiko, kikihimiza umoja na kwamba mgombea huyo ni bora kuliko wa vyama vingine vya siasa.
“Chama chetu kimepitisha jina la mgombea huyu kikijua fika ni mtu makini, mpenda umoja na mchapakazi, abadan msikubali kumpoteza, mchagueni nawaahidi atawasaidia na kuwatumikia  vilivyo,” alisema Mwinyi.
Wagombea wa ubunge katika uchaguzi mdogo jimbo la Chambani kisiwani Pemba ni pamoja na Mattar (CCM), Said Miraji Abdallah (ADC), Yussuf Salum Hussein (CUF) na Sitti Usi Shaib (Chadema).
Kata 26 nchini leo zinafanya uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi na madiwani kwa sababu mbalimbali.
Mchuano mkali unatajwa Arusha ambako kata zake nne Arusha Mjini ambako CCM na Chadema zimesimamisha wagombea ambazo ni Kimandolu, Elerai, Kaloleni na Themi.
Hata hivyo, kata ya Sombetini ambayo aliyekuwa diwani wake, Alphonce Mawazo (CCM) alihamia Chadema, haikuorodheshwa katika kata hizo zinazopaswa kufanya uchaguzi mdogo.
Mbali ya uchaguzi wa kata za Arusha, kata zingine katika halmashauri 21 nchini zinachagua madiwani baada ya nafasi hizo kuwa wazi kutokana vifo, kujiuzulu, kufukuzwa au kuhama chama kwa waliokuwa wakiziongoza.
Kata hizo na halmashauri kwenye mabano ni Stesheni (Nachingwea), Nyampu Lukano na Lugata (Sengerema), Genge Tingeni (Muheza), Ibugule (Bahi), Langiro (Mbinga) na Manchila (Serengeti).
Nyingine ni Iyela (Mbeya), Mbalamaziwa (Mufindi), Ruzewe Mashariki (Bukombe), Mianzini (Temeke), Dalai (Kondoa), Minepa (Ulanga), Makuyuni (Monduli) na Bashnet (Babati).
Mallaba aliongeza kuwa kata nyingine ni Iseke (Singida), Dongobesh (Mbulu), Ng’ang’ang’e (Kilolo), Ifakara (Kilombero), Msanze (Kilosa) na Mnima (Mtwara).
Kutoka Monduli habari zinasema Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa juzi alifunga kampeni Makuyuni kwa wananchi wa kata hiyo kuandamana kwa miguu umbali wa zaidi ya kilometa mbili kuingia mjini humo.
Akizungumza, Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli alitaka wakazi wa kata ya Makuyuni kutoa fundisho kwa Chadema kwa kuinyima kura. 
Alisema Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alikuwa katani hapo na kusema uongo mwingi na aliwambia wakazi wa kata hiyo kuwa dawa ya Mbunge huyo ni kumnyima kura ili ajue kuwa Monduli ina wenyewe.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4617

Trending Articles