Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4500

RUBANI ATAPELI MAMILIONI YA SHILINGI DAR...

$
0
0

Kasi ya utapeli kwa njia ya mtandao nchini, imemkumba na kumwathiri mkazi ya Mbagala, Dar es Salaam, Leonard Abel `Rambo’, baada ya kujikuta akitapeliwa zaidi ya Sh milioni 80 kwa ahadi ya kusomeshewa watoto kwenye shule nzuri nje ya nchi, na hasa Ulaya.

Rambo aliyekuwa anajishughulisha na biashara, alisema hayo alipozungumza na mwandishi baada ya hivi karibuni kuripoti juu ya utapeli unaofanywa na watu wanaodaiwa kuwatafutia kazi Watanzania katika shirika la ndege la Qatar Airways.
Akizungumza kwa hisia, alisema baada ya kusoma habari hiyo, alihamasika kuanika yaliyomsibu, akidai alitapeliwa kiasi hicho cha fedha na mtu aliyemtaja kuwa ni Ladislaus Igambisa na kwamba tayari taarifa hizo ziko kwa makamanda wa Polisi wa mikoa ya Temeke na Kagera.
Akifafanua juu ya tukio hilo lililochangia yeye na familia yake kuishi maisha magumu, na hata kushindwa kusomesha mtoto wake aliyefaulu kujiunga na sekondari, alisema alikutana na mtu huyo mwaka 2011 akiwa anajishughulisha na biashara ya nguo na vitu vingine.
“Siku ya kwanza alifika dukani kwangu kununua viatu vyake na vya mwanawe. Kesho yake alirudisha viatu vya mwanawe akidai vilimbana hivyo kuomba abadilishiwe, tangu hapo aliendelea kujenga mazoea nami huku akinunua bidhaa mbalimbali na baadaye akawa rafiki.
“Baada ya kuzoeana, aliniambia kuwa anafanya kazi ya urubani na pia ni mwanausalama wa Taifa anayefanya pia kazi ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) na huwa anasafiri mara kwa mara,“ alisema.
Alisema mazoea yalishamiri baada ya mtuhumiwa huyo kudai alisafiri (sehemu ambayo hakuitaja) na kuna siku alimpigia simu akimtaka amsaidie kumpa mkewe Sh 50,000 kwa kuwa yuko mbali na hana sehemu ambayo angeweza kumtumia fedha mkewe.
“Nilikubali na  aliporejea alinirudishia, akasema kutokana na upendo niliouonesha kwa mkewe, inabidi kufungua ukurasa mpya wa ukaribu na hata kutaka familia zetu zitembeleane na ikiwezekana kusaidiana katika shida na raha.
“Nilipokwenda kumtembelea kwake eneo la Jet (Kwa Gude), tulizungumza mengi na baadaye akaniuliza kama naweza kusomesha watoto wangu katika shule nzuri. Nilimjibu siwezi, yeye akasema atanifanyia wema ambao sitasahau kwa kuwa nilimsaidia mkewe yeye akiwa safarini,” alisimulia Rambo.
Aliongeza, kuwa baada ya kauli hiyo mtuhumiwa alimletea barua akidai inatoka Kanisa Katoliki ya kutafuta wafadhili wa kusomesha watoto nje ya nchi.
“Baada ya kujaza barua hiyo niliituma kwa anuani aliyonipa, akiniambia inakwenda kwa Mfadhili Mkuu wa Shirika la CRS Apostles, na baada ya hapo nilipata barua mfululizo kupitia mtandao zikinitaka kutoa viwango tofauti vya fedha, ili kuwezesha watoto wakasome Scotland, Canada na Italia,” alisema Rambo.
Aidha, alisema kwa muda wote ambao alikuwa akitafutiwa wafadhili, alikuwa akiwasiliana kwa njia ya simu hasa usiku wa manane na watu mbalimbali wakijitambulisha kuwa wakurugenzi wa kampuni ya kutafuta wafadhili.
“Ilikuwa ni mateso makubwa, kwani watu hao kwa muda wa miaka mitatu mfululizo walinitaka niwaamshe watoto wangu kila siku saa nane usiku, ili waendelee kuzungumza na kuwauliza kama mimi (baba yao) nimetekeleza masharti ambayo wamekuwa wakinipa mara kwa mara, hali iliyonikuta nikimaliza kiwango hicho chote cha fedha.
Akifafanua, alisema alikuwa amepewa masharti ya kuwa anatuma fedha za kigeni nje ya nchi ambazo alizipata baada ya kuuza nyumba zake mbili; moja Dar es Salaam na nyingine Mwanza na kujikuta akifunga maduka yake mawili, la vipodozi na la nguo za kike.
Hali hiyo ilimfanya aishiwe fedha na kushindwa kumalizia hata ujenzi wa nyumba yake aliyokuwa akijenga Dar es Salaam, ambayo alilazimika kuhamia bila kukamilika na ndimo anaishi sasa na familia yake.
“Hata hivyo, niligundua kuwa nimetapeliwa kwa barua yao ya mwisho ambapo niliamua kwenda Polisi Temeke, nikaonana na Kamanda Engelbert Kiondo, nikamwomba msaada huku nikionesha picha ya mtuhumiwa huyo na Kamanda aliniandikia barua ikinitaka niende Bukoba nilikoambiwa mtuhumiwa wangu yuko wakati huo. Nilikwenda, lakini sikufanikiwa kumpata.”
Akizungumzia tukio hilo juzi, Kamanda Kiondo alisema ni kweli ana taarifa za Leonard au Rambo na aliahidi kuzifanyia kazi kwani anasubiri taarifa kutoka kwa Kamanda wa Polisi wa Kagera, Philip Kalangi.
Kamanda Kalangi akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili kutoka Kagera, alisema hajui tukio hilo kwa kuwa alikuwa likizo kwa takribani mwezi mmoja kuanzia Mei. Hata hivyo alisema atalifuatilia kwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa aliyekuwa anakaimu ukamanda wa mkoa katika kipindi hicho.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4500

Trending Articles