Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4529

MAPATO NA MATUMIZI YA VYAMA VYA SIASA SASA KUKAGULIWA...

$
0
0
Dk William Mgimwa.
Mapato na matumizi ya vyama vya siasa yataanza kukaguliwa katika mwaka ujao wa fedha.

Waziri wa Fedha Dk William Mgimwa alisema hayo bungeni jana wakati akisoma hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha bungeni.
Kwa mujibu wa Mgimwa, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu itaanza kazi hiyo mwaka ujao wa fedha kukidhi matakwa ya sheria ya vyama vya siasa vyote.
Aidha Dk Mgimwa alisema yanaendelea kufanyika mazungumzo na Msajili wa Vyama vya Siasa juu namna ya kutekeleza Sheria ya Gharama ya Uchaguzi.
Kutekelezwa kwa sheria hiyo, kutakidhi kiu ya watu mbalimbali ambao wamekuwa wakivinyooshea vyama vya siasa vidole vikidaiwa kuwa na matumizi mabaya ya fedha ndani yake.
Wapo ambao wamewahi kupendekeza kazi hiyo ya ukaguzi ifanywe na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ikielezwa kwamba licha ya baadhi ya vyama kupata fedha nyingi kutoka kwa wafadhili wa ndani na nje, matumizi yao si mazuri.
Miongoni mwa waliowahi kutaka hilo lifanyike, ni Waziri mstaafu, Joseph Warioba ambaye aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari akisema mambo ya fedha ndani ya vyama, huzungumzwa pale wanapogombana wao kwa wao licha ya kwamba mapato na matumizi ya fedha za umma za aina yoyote ni jambo la msingi katika nchi ya kidemokrasia.
Serikali imesema katika kuboresha usimamizi wa deni la Taifa inakamilisha uanzishwaji wa Idara ya Usimamizi Madeni, pia inaandaa rasimu ya utaratibu wa mfumo wa ununuzi wa magari kwa pamoja kwani hilo ni eneo ambalo linatumia fedha nyingi za umma.
Pia imesema Pato la Taifa limeendelea kuimarika na kufikia ukuaji wa asilimia 6.9 mwaka 2012 ikiwa ni zaidi ya lengo la asilimia 6.8 na Mfumko wa Bei umepungua kutoka asilimia 18.7 Aprili mwaka jana hadi asilimia 9.4 Aprili mwaka huu.
"Deni la Taifa linajumuisha mikopo ya nje na mikopo ya ndani, Wizara iliendelea kusimamia ulipaji wa deni la Taifa ambapo katika kipindi cha Julai 2012 hadi Aprili 2013 malipo yalifikia Sh bilioni 1,666.77.
"Kati ya hayo, malipo ya deni la nje ni Sh bilioni 213.57 na malipo ya deni la ndani Sh bilioni 1,453.20. Aidha katika kuboresha usimamizi wa deni la Taifa, Wizara inakamilisha uanzishwaji wa Idara Usimamizi wa Madeni, ambayo itaanza kazi mwaka ujao wa fedha.
"Pamoja na mambo mengine itakuwa na jukumu la kujenga uwezo wa kufanya upembuzi yakinifu na kuhakikisha kuwa uwezo wa usimamizi madhubuti wa Deni la Taifa unajengwa na kuimarishwa," alisema Dk Mgimwa.
Dk Mgimwa alisema ununuzi wa magari ni moja ya maeneo ambayoÊ yanatumia fedha nyingi za umma. Kutokana na hilo Serikali imeona kuwa kuna umuhimu wa kuweka utaratibu bora utakaowezesha kupata thamani ya fedha katika ununuzi pamoja na matumizi ya magari yake.
Alieleza kuwa ununuzi wa magari kwa sasa umekuwa ukifanywa kila wizara, idara zinazojitegemea, taasisi za Serikali, halmashauri na ofisi mikoa kwa kila moja kuandaa mchakato wa ununuzi wake.
Alisema ununuzi huo umesababisha kuwepo kwa aina nyingi za magari na kwa bei zinazotofautiana baina ya taasisi zake na hivyo sasa itabidi Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini (GPSA) ihusike.
"Wizara imeandaa rasimu ya utaratibu wa mfumo wa ununuzi wa magari kwa pamoja, ambapo GPSA itahusika na jukumu hili. Utaratibu huu utaanza kutumika baada ya kupitishwa na mamlaka zinazohusika," alisema Waziri Mgimwa.
Kuhusiana na mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Dk Mgimwa alisema imekuwa na mafanikio, lakini pia kuna changamoto mbalimbali ikiwemo wanachama kulalamikia kiwango kidogo cha mafao kitolewacho na baadhi ya mifuko hiyo pale wanapostaafu.
"Katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo, Serikali kupitia Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Hifadhi ya Jamii imepanga kutathmini uwezo wa mifuko yote ya hifadhi ya jamii na kupendekeza viwango vya mafao na kuhakikisha kwamba mifuko hiyo inakuwa endelevu," alisema.
Kuhusu usimamizi wa uchumi, Waziri Mgimwa alisema katika mwaka 2012 pato la Taifa liliendelea kuimarika na kufikia ukuaji wa asilimia 6.9 ikilinganishwa na asilimia 6.4 mwaka 2011 ikiwa ni zaidi ya lengo la asilimia 6.8 mwaka 2012.
"Aidha Benki Kuu ya Tanzania ilipandisha kiwango cha chini cha akiba ya amana za Serikali katika benki kutoka asilimia 30 hadi 40 pamoja na kupunguza kiwango cha kuhodhi fedha za kigeni kulingana na mitaji yao kwa benki kutoka asilimia 10 hadi asilimia 7.7 kuanzia Desemba 2012.
"Hatua hizi zilisaidia kupunguza kiwango cha mfumuko wa bei kutoka asilimia 18,7 Aprili mwaka 2012 hadi asilimia 9.4 mwezi Aprili mwaka 2013 pamoja na kusaidia kuimarika kwaÊ kiwango cha ubadilishaji wa Shilingi dhidi ya dola ya Marekani," alisema Waziri.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4529

Trending Articles