Serikali imeunda kikosi maalumu kitakachoratibu matumizi ya mitandao ya kompyuta na kitakuwa na jukumu la kufuatilia na kudhibiti uhalifu wa kimtandao nchini.
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, alisema hayo jana katika hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka ujao wa fedha.
Alisema katika kukabiliana na uhalifu wa kimtandao, imeandaliwa Sheria ya Usalama wa Mtandao na kwamba rasimu ya awali tayari na kinachofuata sasa ni kuwasilishwa kwa wadau ili kupata maoni.
Profesa Mbarawa, alisema hatua ya kuunda kikosi hicho inatokana na kupanuka kwa matumizi ya mtandao katika nyanja mbalimbali za maisha.
Wizara hiyo iliomba bunge liidhinishe matumizi ya Sh 63,147,599,460.
"Serikali imeunda kikosi kitakachoratibu na kufuatilia matumizi ya mitandao ya kompyuta (Computer Emergency Response Team-CERT). Tayari kikosi hicho kimeanzishwa na kinafanya kazi ndani ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
"Aidha kikosi hicho kimepewa jukumu la kufuatilia na kudhibiti uhalifu wa kimtandao nchini kushirikiana na wadau wengine ulimwenguni," alisema na kuongeza kuwa kutokana na kuundwa kikosi hicho kinachofuata sasa ni mafunzo ya kujenga uwezo wa rasilimali watu kwa ajili ya kikosi hicho.
Alieleza kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na SADC inaandaa Sheria ya Usalama wa Mtandao.
"Rasimu ya awali ya sheria imeandaliwa, hatua inayofuata ni kuwasilishwa kwa wadau kwa ajili ya kupata maoni. Kwa kuanzia sheria hiyo itahusisha masuala ya uhifadhi wa taarifa, biashara ya mtandao na matumizi salama ya mtandao," alisema Waziri na kuongeza kuwa wizara yake imeandaa Sera ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia ambayo tayari imeridhiwa na Baraza la Mawaziri.
"Mchakato wa kuandaa sheria ya kuendeleza sayansi nchini upo katika ngazi ya wadau kutoa maoni," alisema Waziri huyo.
Kuhusu uzimaji wa mitambo ya analojia, alisema umefanyika katika miji ya Dar es Salaam, Dodoma, Tanga, Mwanza, Moshi, Arusha na Mbeya na hivyo kukamilisha awamu ya kwanza ya usitishaji wa urushaji wa matangazo kwa kutumia mitambo ya analojia.
Alisema tathmini ya awali ya uzimaji wa mitambo ya analojia kwa Dar es Salaam inaonesha kuwa inakadiriwa zipo runinga zipatazo 600,000 kwenye kaya na kwamba hadi kufikia Desemba mwaka jana zaidi ya runinga 250,000 kati ya 600,000 zilikuwa katika mfumo wa dijitali kupitia teknolojia ya kupokea matangazo ya satelaiti.
Idadi ya runinga zilizobaki, 350,000 ndizo zilizohusika na mabadiliko ya teknolojia kutoka analojia kwenda dijitali. Kwa mujibu wa waziri, runinga hizo 600,000 zilizokadiriwa hazijumuishi zilizoko kwenye hoteli, nyumba za starehe na maeneo mengine.
"Kwenye miji yote mingine mitambo ya analojia bado ipo hewani na itakuwa hivyo mpaka pale mawimbi ya dijitali kwenye miji hiyo yatakapoanza kupatikana baada ya kukamilisha usimikaji wa mitambo na kuanza kufanya kazi," alisema.
Wabunge wameendelea kuzinyooshea vidole kampuni za simu za mkononi wakizishutumu kuibia wananchi. Mbunge wa Chonga, Haroub Mohammed Shamisi (CUF) ni miongoni mwa waliosema serikali inakosa mapato mengi ya kodi kwenye kampuni hizo.
Alitoa mfano kwamba amewahi kuibiwa kwa kununua kifurushi cha intaneti lakini hakupata na alipofuatilia aliambiwa simu yake aina ya Blackberry haipo katika ofa hiyo.
Mbunge huyo alilalamika kwamba kama yeye mwakilishi wa wananchi anatapeliwa hivyo, basi ni hatari kwa wananchi wengine na kueleza kuwa kiasi alichotapeliwa na kampuni hiyo ya simu ni Sh 15,000 na kwamba fedha hizo na zaidi wamekuwa wakiibiwa karibu kila siku wananchi mbalimbali.
Pia Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu, alimuunga mkono Shamisi aliyesema fedha nyingi zipo katika kampuni za simu na kama sheria itawekwa vizuri, serikali itapata kodi ya kutosha tofauti na sasa ambapo uwezekano wa kupata fedha hizo ni mdogo.
Zungu alitoa mfano kwa mtu anayenunua vocha ya Sh 10,000 ambayo serikali inatakiwa ipate Sh 3,000 kama akipiga simu, lakini ikitokea mtu huyo hapigi simu ni ngumu kuchukua kodi hiyo hali aliyosema inatakiwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ijipange vizuri kwa kodi kuhusiana na mambo ya simu za viganjani.
Mbunge wa Nkenge, Assumpta Mshama (CCM) alisema Watanzania wanaibiwa kutokana na sheria kutokuwa vizuri juu ya mambo ya kodi kwenye simu za mkononi.
Akisoma maoni ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu kwa wizara hiyo, mjumbe wa kamati hiyo ambaye ni Mbunge wa Tunduru, Mtutura Abdallah Mtutura (CCM), alisema mfumo wa kuratibu huduma ya mawasiliano nchini unalenga kuhakikisha mapato yatokanayo na huduma za sekta za mawasiliano yanajulikana vyema na yanachangia kikamilifu pato la taifa.