![]() |
Waokoaji wakishughulikia kuwatoa majeruhi wa ajali hiyo. |
Ndege moja imeanguka wakati ikijaribu kutua kwenye uwanja ulioko milimani huko kaskazini mwa Nepal mapema jana, na kujeruhi watu wote 21 waliokuwamo ndani yake.
Wanne kati ya waliojeruhiwa wako katika hali mbaya, ofisa wa polisi Bhim Bahadur Chand alisema.
Hakuna aliyepoteza maisha katika ajali hiyo.
Abiria tisa ni watalii kutoka Japan, na wafanyakazi watatu wa ndege hiyo na abiria wengine wote ni raia wa Nepal.
Ndege hiyo inayomilikiwa na shirika la serikali la Nepal Airlines ilikuwa ikijaribu kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Jomsom, takribani maili 125 kaskazini mwa Katmandu, ndipo ikajibamiza kwenye kingo za mto Kaligandaki.
Waliojeruhiwa walikimbizwa kwenye hospitali za mjini humo, na wote waliopata majeraha makubwa walisafirishwa kwa ndege hadi mji jirani wa Pokhara kwa matibabu.
Eneo hilo ni maarufu kwa watalii wa kigeni wanaotembelea eno la Mlima Annapurna na mahujaji wa Kihindu wanaotembelea hekalu la Muktinath.
Watu 15 walikufa Mei, mwaka jana pale ndege ilipoanguka wakati ikijaribu kutua kwenye uwanja huo wa ndege.
Mvuto wa milima ya Himalaya huvutia zaidi ya watalii 100,000, wakiwamo Waingereza 40,000, kila mwaka wanaokwenda nchini Nepal.
Namba ya wanaotembelea Mlima Everest imeongezeka maradufu tangu kukoma kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo mwaka 2006 - lakini kuanguka kwa ndege kumekuwa kukiwatisha mara kwa mara watalii katika nchi za Kiasia.
Marubani na wataalamu nchini Nepal wanahofia ajali zaidi zitatokea katika nchi hiyo ambako kushindwa kwa siasa na taratibu duni zinaporomosha sekta yake ya utalii.
Marubani wako katika shinikizo kubwa mno kutoka kwa mabosi zao wakati wa vipindi vya kazi nyingi na kwamba Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Nepal (CAAN) haina uwezo wa kushughulikia matatizo yanayoathiri usalama.
Wanahofia kwamba msongamano mkubwa katika eneo la Everest unaweza kusababisha mgongano angani.
Mamlaka ya Usalama wa Anga barani Ulaya imeiandikia CAAN kutaka kujua kilichofanyika kuhusu kuboresha usalama.
Baadhi ya wataalamu wanaamini kwamba moja au zaidi ya madhirika ya ndege ya Nepal hivi karibuni yatawekwa kwenye orodha ya wanaotakiwa kuadhibiwa ya Umoja wa Ulaya.