![]() |
Mabaki ya ghorofa hilo lililoporomoka makutano ya Mitaa ya Indira Gandhi na Morogoro. |
Upelelezi wa kesi ya kuua bila kukusudia, kutokana na kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 katika mtaa wa Indira Gandhi, Dar es Salaam, inayowakabili watu 11 akiwemo mmiliki wa jengo hilo, Razah Lazah, haujakamilika.
Wakili wa Serikali Bernard Kongola, alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Devotha Kisoka, wakati kesi hiyo ilipotajwa.
Hakimu Kisoka aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 12 mwaka huu, itakapotajwa tena na washitakiwa wataendelea kuwa nje kwa dhamana.
Washitakiwa wote waliachiwa kwa dhamana baada ya kusaini hati ya Sh milioni 20, kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, ambao kila mmoja alisaini hati ya Sh milioni 20. Waliwasilisha hati zao za kusafiria na wamezuiwa kusafiri bila kuwa na kibali cha mahakama.
Mbali na Lazah, washitakiwa wengine ni Diwani katika Manispaa ya Kinondoni, Ibrahim Mohamed (59), vigogo wa Manispaa ya Ilala ambao ni Mhandisi Mkuu, Charles Salu (48), Mhandisi wa Majengo, Godluck Mbaga (35) na Mkurugenzi Mkuu wa Mkaguzi wa Majengo, Willibrod Wilbard (42).
Wengine ni Mhandisi, Mohamed Swaburi (61), Mhandisi Mshauri, Zonazea Oushoudada (60), Mkadiriaji Ujenzi, Vedasto Nziko (59), Msanifu Majengo, Michael Hema (59), Msajili Msaidizi AQRB, Albert Mnuo na Ofisa Mkuu Mtekelezaji OQRB, Joseph Ringo.
Inadaiwa kuwa Machi 29, mwaka huu katika mtaa huo, washitakiwa waliwaua bila ya kukusudia Yusuph Mohamed, Kulwa Alfan, Hamada Musa, Kessy Manjapa, Khamis Mkomwa, Boniface Benard. Wengine ni Suhail Ally, Salmani Akbar, Seleman Haji, Seleman Mtego, Sikudhani Mohamed.
Wengine ni Ahmed Milambo, Salum Mapunda, Suleiman Rashid na John Majewa, Mussa Mnyamani, David Severin Herman, William Joackim, Abdulrahman Mwiha, Emmanuel Christian, Mmanyi Ngadula, Adivai Desiki, Emmanuel Greyson na Augustino Kasiri.