Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4605

DEREVA WA BODABODA ASOMEWA MASHITAKA YA MAUAJI BOMU LA KANISANI ARUSHA...

$
0
0
Kamanda Liberatus Sabas.
Wakati mtuhumiwa wa mlipuko wa bomu kanisani Arusha, Victor Ambrose (20), akifikishwa mahakamani raia wanne kutoka nchi za Kiarabu, waliokamatwa kwa tuhuma hizo hizo wameachiwa huru.

Ambrose ambaye ni dereva wa bodaboda, alifikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha na kusomewa mashtaka mawili ya mauaji, na kujaribu kuua mbele ya Hakimu Devotha Kamuzora.
Hata hivyo, ilibainika pia kuwa raia hao wa kigeni waliokuwa wanashikiliwa sambamba na Ambrose si wote wanatoka Saudi Arabia kama ilivyotangazwa awali, bali watatu wanatoka Falme za Kiarabu (UAE) na mmoja tu ndiye Msaudia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema jana kwamba uchunguzi wa kina uliofanywa na timu ya upelelezi iliyoshirikisha Shirika la Ujasusi la Marekani (FBI) na Shirika la Kimataifa la Polisi (Interpol), umebaini raia hao wa kigeni hawakuhusika na tukio hilo.
Uchunguzi huo ulibaini wageni hao ni raia wema na wengine wanafanya kazi katika taasisi za Serikali zinazoheshimika nchini kwao.
Alitaja raia watatu wanaotoka UAE ambao walidhaniwa ni Wasaudia kuwa ni Abdul Aziz Mubrak (30) ambaye ni mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato ya UAE, Fouad Saleem Ahmed (29) anayefanya kazi Kikosi cha Zimamoto na Saeed Abdalla Saad (28), ambaye ni askari Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani.
Kwa mujibu wa Kamanda Sabas, Msaudia kati ya watuhumiwa hao ni  Al- Mahri Mohseens (29) pekee, ambaye ni raia wa kawaida wa nchi hiyo, aliyekuwa akipita nchini.
Kabla ya kuachiwa huru, jalada la tukio hilo lilifikishwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), ambapo ofisi hiyo ilielekeza watuhumiwa hao wakabidhiwe kwa  Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Arusha, ili ijiridhishe kama hakuna utaratibu wowote za kiuhamiaji  uliokiukwa na wageni hao, wakati walipoingia nchini.
“Naomba nisisitize, kwamba raia hawa wameachwa huru, kwa sababu hawakuhusika na wameingia nchini kihalali na walifuata utaratibu wote,’’ alisema Kamanda Sabas.
Kaimu Ofisa wa Uhamiaji Mkoa wa Arusha, Vitalis Mlay, alisema raia hao wanne waliingia nchini kihalali,  kwa ndege ya Shirika la Ndege la Qatar  saa 4 asubuhi na ni mara ya kwanza kuja nchini.
Pia aliongeza kuwa raia hao walipelekwa Dar es Salaam wakiwa chini ya ulinzi mkali, ili wasafirishwe kurudi kwao.
Kwa upande wa Ambrose, wakati akisomewa mashitaka hayo, Wakili wa Serikali, Zakaria Elisaria, alidai kuwa alifanya makosa mawili ya kuua na kujaribu kuua watu kadhaa Mei 5 kati ya saa 4.30 na saa 5 asubuhi. Hata hivyo Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Mei  27.
Akizungumzia watuhumiwa wengine waliokamatwa katika kamatakamata iliyotokana na tukio hilo, Kamanda Sabas alisema bado wanaendelea kuhojiwa na Polisi ambapo maelezo yao hayajatosha kufikishwa mahakamani.
Alitaja watuhumiwa hao kwamba ni dereva wa bodaboda, Yusuph Lomayani ‘Josee’ (18), George Silayo (23), Mohamed Said (38), mkazi wa Ilala, Dar es Salaam, Mohamed Saada (38) na mkazi wa mtaa wa Bondeni, Arusha, Jasm Mubarak (29).
"Watuhumiwa wengine wanahojiwa na Polisi mbali na huyo aliyefikishwa mahakamani jana. Pia uchunguzi dhidi ya watuhumiwa waliosalia unaendelea na kwa sasa tuna wataalamu kutoka Kenya na Uganda tunaoshirikiana nao katika upelelezi wa shauri hilo,” alisema.
Aliwasihi wananchi kutoa taarifa, ili kufichua watu waliohusika na mtandao huo wa kigaidi na kuahidi atakayefichua atapewa Sh milioni 50.
Hadi  sasa kwa maelezo ya Kamanda Sabas, majeruhi wa tukio hilo la bomu, 31 wanaendelea kupata matibabu katika hospitali mbalimbali, huku 19 kati yao wakiwa hospitali za Mount Meru, wanne St Elizabeth na wengine wanane Muhimbili, Dar es Salaam.
Mlipuko huo ulisababisha watu watatu kupoteza maisha na 31 kujeruhiwa.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4605

Trending Articles