Kaya 2,857 wilayani Kilosa zimekosa makazi kutokana na nyumba 379 kubomoka na nyingine 997 kuzingirwa na maji yaliyotokana na mafuriko yaliyokumba wilaya hiyo ya Mkoa wa Morogoro.
Mafuriko hayo yametokana na mvua kubwa zilizonyesha katika safu za milima ya Wilaya za Kongwa na Mpwapwa mkoani Dodoma na maji yake kujaa mto Mkondoa unaokatisha katika mji wa Kilosa.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, John Henjewele alisema hatua za awali ambazo zimechukuliwa ni pamoja na kuhifadhi kwa muda waathirika wa mafuriko kwenye shule ya Msingi ya Lamlilo, mahakama ya mwanzo na katika ofisi ya mtendaji kata ya Magomeni.
Aidha alisema, mahitaji ya awali kwa waathirika hao yameshaandaliwa yakihusisha chakula, maji, dawa wakiwa eneo hilo kwa muda wakisubiri kuhamishiwa katika kambi maalumu zitakazotengwa.
Alitoa taarifa hiyo juzi kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Rajab Rutengwe aliyekwenda kukagua maeneo yaliyoathiriwa.
Henjewele alisema mafuriko hayo yalitokea usiku wa kuamkia Januari 5, pia yameathiri miundombinu ya barabara ya Kilosa – Mikumi ambayo kwa sasa haipitiki. Pia imeharibu mashamba huku kata ya Magomeni ikitajwa kuathirika zaidi.
Pia nyumba 33 zilizopo katika Kata ya Berega mapaa ya majengo ikiwemo vyoo vya shule za Msingi Kiegeya, Mugugu na Berega, yameezuliwa.
Diwani wa Kata ya Magomeni, Abdallah Huwel alishauri serikali kujenga tuta upande wa pili wa mto Mkondoa. Kumbukumbu zinaonesha mafuriko makubwa yalitokea mwaka 1964 na 1978, 1997; Desemba 2009 na kuendelea hadi Januari, 2010 na kusababisha vifo vya watu wawili. Uliathiri watu 23,980 sawa na kaya 5, 605.