Wakimbizi 115,138 wanaoishi katika makazi ya Mishamo na Katumba mkoani Katavi, waliopewa uraia wa Tanzania, wana haki zote kama Watanzania wa kuzaliwa ya kuwapigia kura madiwani , wabunge na rais , katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Makazi ya Katumba wilayani Mlele, Athman Igwe katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Rukwa (RCC).
Alisema hayo alipokuwa akijibu swali la Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani humo, Laurent Magweshi, aliyetaka kujua iwapo wakimbizi waliopewa uraia nchini, wana sifa ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba mwaka huu.
“Wakimbizi hao sasa ni Watanzania wapya na wana haki kama walizonazo Watanzania wa kuzaliwa ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao,“ alifafanua.
Aliongeza kuwa wanayo haki pia ya kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura na aliwahamasisha kujitokeza kwa wingi, kujiandikisha ili waweze kuipigia kura Katiba inayopendekezwa Aprili 30 , mwaka huu .
“Watanzania hawa wapya wanayo haki ya kuchagua na kuchaguliwa katika nafasi zote za uongozi ikiwemo nafasi ya ubunge, lakini hawaruhusiwi kugombea nafasi ya urais,” alisisitiza
Alibainisha kuwa wakimbizi wapatao 115,138 wanaoishi kwenye Makazi ya Mishamo na Katumba, wamepewa uraia wa Tanzania, katika mpango wa ugawaji vyeti unaoendelea, ambapo 62,544 wanatoka makazi ya Katumba wilayani Mlele na 52,594 makazi ya Mishamo wilayani Mpanda.
Akiwasilisha taarifa ya ugawaji wa vyeti vya Watanzania wapya waliokuwa wakiishi kwenye mkazi hayo, Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Sekretarieti ya Mkoa, Ignas Kikwala alisema makazi ya Katumba yalipokea wakimbizi 2,800 mwaka 1973 na mwaka 1978 Serikali ilianzisha Kambi ya wakimbizi ya Mishamo ikiwa na wakimbizi 12,000 .
Ugawaji vyeti kwa Watanzania hao ulianza Novemba 26, mwaka jana na utakamilika Aprili 30 mwaka huu kwa makazi ya Katumba na Mishamo na Ulyankulu mkoani Tabora .