Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro imempandisha kizimbani Josephat Asenga (47) mhasibu wa kujitegemea ambaye ni padri feki mkazi wa mtaa wa Lusanga, kwa mashitaka ya udanganyifu na kujifanya padri wa Kanisa Katoliki.
Mbele ya Hakimu Mkazi Agripina Kimanze, wakili wa Serikali Gloria Rwakibarika alidai kuwa mshitakiwa kwa nyakati tofauti kati ya Mei mwaka jana na Machi 5 mwaka huu, majira tofauti alifika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Maria Mtakatifu Modeko na kudanganya kuwa yeye ni padri.
Alidai kuwa mshtakiwa huyo alijitambulisha kwa Padri wa Parokia ya Maria Mtakatifu Modeco, Padri Maliti Joseph Dyfrig kwa nia ya kutapeli huku akijua kuwa ni kinyume cha sheria.
Wakili Rwakibarika aliendelea kudai kuwa Asenga alifika parokiani hapo na kujitambulisha kuwa yeye ni padri wa kanisa hilo kinyume na kifungu cha sheria namba 369(1) na kifungu cha sheria namba 35 vya sheria ya kanuni za adhabu sura ya 16 ya mwaka 2002. Wakili huyo alisema kuwa upelelezi juu ya shitaka hilo haujakamilika.
Mshitakiwa Josephat Asenga amekana shitaka lake, hata hivyo mahakama hiyo chini ya hakimu wake ilisema dhamana juu ya mshtakiwa huyo iko wazi, lakini kwa masharti ya kutakiwa kuwa na wadhamini wawili wa uhakika mmoja wapo akiwa ni mtumishi wa serikali huku wakiwa na Sh milioni 1 kila mmoja.
Mshitakiwa huyo alishindwa kutimiza masharti hayo ya dhamana, hatua iliyomfanya arejeshwe rumande. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 25 mwaka huu shitaka lake litakapotajwa tena mahakamani hapo.