Askari aliyekuwa dereva wa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) Manyoni mkoani hapa, Aloyce Alibinus amejiua kwa kujipiga risasi mdomoni na kutokea kisogoni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka (pichani) alithibitisha tukio hilo huku akisema askari huyo alijiua jana majira ya asubuhi nyumbani kwake kwa kutumia bunduki ya jeshi hilo iliyokuwa na risasi nane.
Alisema kabla ya kujiua, askari huyo aliyekuwa amejipumzisha nyumbani kutokana na kusumbuliwa na homa, alitoka na kwenda kwenye ghala la silaha na kuomba apewe bunduki moja kwa kile alichodai kuwa alikuwa na safari ya kikazi na bosi wake ambaye ni OCD.
Alieleza kuwa mtunza ghala hilo alimwamini na kumpatia bunduki hiyo yenye risasi nane ambayo alikwenda nayo moja kwa moja nyumbani kwake na kujifungia kisha kufungulia redio kwa sauti ya juu.
Aliongeza kuwa, askari huyo alielekeza mtutu wa bunduki hiyo mdomoni kwake na kujifyatulia risasi ambayo ilipitiliza hadi kisogoni hivyo kusababisha kifo chake papo hapo.
Alisema ingawa uchunguzi wa kina unaendelea kufanywa juu ya chanzo cha askari huyo kuamua kukatisha uhai wake kwa kujiua, lakini ujumbe wa maandishi aliouacha mezani umelitaka Jeshi la Polisi kutomsumbua mtu yeyote, akisema amejiua kwa utashi wake.