Wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (TAZARA) wamelipwa mishahara yao ya miezi minne waliyokuwa wakidai .
Hatua hiyo imemaliza mgogoro uliodumu muda mrefu kati ya mamlaka hiyo na wafanyakazi.
Tangu Aprili hadi Agosti mwaka huu , wafanyakazi hao walikuwa katika mgogoro na Tazara wakishinikiza kulipwa fedha zao, hatua ambayo ilisababisha kutishia kugomea kazi mara kwa mara.
Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli (TRAWU) Elasto Kiwele, alimwambia mwandishi jana kwamba mishahara hiyo imelipwa na kubakia madai ya Agosti ambayo hayakuwepo katika madai hayo ya awali.
“Malipo yaliyotolewa ni kwa ajili ya miezi ya Aprili, Mei, Juni na Julai, deni lililobaki ni la mwezi ulioisha ambao hata hivyo kimsingi suala lake halikuwepo katika madai tuliyokuwa tukiyalalamikia,” alisema Kiwele.
Katibu huyo wa Trawu aliitaka Menejimenti ya Tazara kuweka mipango mizuri ya utendaji kazi ili kuwawezesha wafanyakazi kutekeleza majukumu yao ya uzalishaji na hivyo kuongeza ufanisi wa mamlaka hiyo.