Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4529

WATU 29 WAUAWA KATIKA SHAMBULIZI LA KIGAIDI KENYA

$
0
0
Watu wenye silaha wameua watu 29 katika mashambulizi mawili tofauti eneo la Pwani ya Kenya.
Shambulizi la kwanza limefanyika katika  eneo la Hindi na lingine Gamba, karibu na mpaka wa Kenya na Somalia.
Tayari kundi la kigaidi la al-Shabaab kutoka Somalia limekiri kuhusika na mashambulizi hayo, yaliyofanywa usiku wa kuamkia jana katika maeneo hayo ya Pwani.
Kati ya watu hao 29, watu tisa walipoteza maisha katika shambulizi lililofanywa katika eneo la Hindi katika Jimbo la Lamu; na waliobakia walipoteza maisha yao katika eneo la Gamba, jirani na Jimbo la Tana River. Majimbo yote hayo yapo Kaskazini mwa Mombasa.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kenya, Mwenda Njoka, mauaji hayo yamefanyika wakati Wakenya, hasa wakazi wa eneo la Hindi, wakiwa katika msiba uliosababishwa na shambulizi lingine kama hilo, lililoua zaidi ya watu 60 wiki mbili zilizopita.
Katika shambulizi lililoua watu 60 lililotokea eneo la Mpeketoni   katika eneo hilo la Hindi, watu wenye silaha walishambulia hoteli, Kituo cha Polisi na watu waliokuwa wakiangalia mechi ya Kombe la Dunia.
 “Kulikuwa na mashambulizi mawili katika majimbo ya Lamu na Tana River usiku. Shambulizi la Lamu kuna watu tisa wamekufa na Tana River wamekufa watu 20. Idadi inaweza kuongezeka,” alisema Njoka.
Maofisa wa Polisi walisema kundi la watu 10 mpaka 15, walivamia eneo la Hindi lililoko kilometa 15 kutoka Lamu na karibu ya Mji wa Mpeketoni, ulioshambulia mwezi uliopita saa nne usiku juzi.
“Walifika na kuanza kushambulia watu hovyo hovyo,” alisema mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa eneo hilo, Abdallah Shahasi.
Shahasi aliongeza: “Washambuliaji walikuwa vijana waliovaa sare za msituni na walikuwa wakizungumza kwa lugha ya Somalia.”
Wavamizi hao wanadaiwa kuvamia Kituo cha Polisi na kuvunja chumba cha mahabusu na kutorosha watuhumiwa, waliokuwa wakishikiliwa.
“Wamewaua wenzetu (askari) na kuwatorosha watu waliokuwa wanashikiliwa. Baadhi ya watu hao walikuwa wakihusishwa na mashambulizi ya Mpeketoni yaliyotokea wiki mbili zilizopita.
Bado hatuna idadi ya watuhumiwa waliotoroshwa mpaka tutakapohakiki vitabu vya usajili,” alisema polisi moja, ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Akizungumzia tukio hilo, Naibu Kamishna wa Polisi, Mike Kimoko  alisema katika mashambulizi hayo, askari Polisi aliyekuwa zamu aliuawa, kabla ya kuwatoa nje watu watano, walikuwa wakishikiliwa Polisi na kuwaua kwa risasi.
Mbali na mahabusi watano kuuawa, wavamizi hao walishusha watu watatu kutoka kwenye gari, lililokuwa limefika katika kituo hicho, na kuwaua kabla ya kutokomea kwenye vichaka.
“Watu wenye silaha nzito walivamia mahabusu majira ya saa tano usiku na kumuua askari Polisi, mahabusi watano na raia watatu walikuwa ndio wanafika kituo cha Polisi,” alisema Kimoko.
Akisimulia namna polisi aliyekuwa zamu alivyouawa, Kimoko alisema aliuawa katika mapambano ya  kurushiana risasi na watu hao, kabla ya kuingia kwenye chumba cha mahabusu.
Kimoko alisema washambuliaji, walitumia fursa ya kuwapo giza kwenye Kituo cha Polisi, ambacho hakijaunganishwa umeme, na mpaka sasa imekuwa ngumu kutaja idadi ya washambuliaji hao na hakuna mtuhumiwa yeyote aliyekamatwa.
Kamishna wa Jimbo la Lamu, Miiri Njenga alisema baadhi ya mali na ofisi za Serikali, zimeharibiwa vibaya.
Mwanamke mmoja alidai kuwa washambuliaji hao, waliteketeza nyumba yake. Pia, alidai walisema kuwa hawataki kuua wanawake.
“Wamesema wanafanya mashambulizi kwa sababu ardhi wa Waislamu imechukuliwa,” alidai mwanamama huyo.
Tayari kundi la kigaidi la al Shabaab, lenye asili yake Somalia na ambalo limekuwa likihusika na mashambulizi mengi nchini Kenya, limetangaza kuhusika na mashambulizi hayo ya juzi usiku.
"Washambuliaji wamerejea salama kwenye ngome yao,” alisema msemaji wa al-Shabaab, Abdulaziz Abu Musab.
Kutokana na mashambulizi hayo ya Hindi na Gamba, Naibu Rais wa Kenya, William Ruto amefuta ziara yake ya jana katika mji wa Mpeketoni.
Ruto alipanga kufanya ziara eneo hilo na kuhudhuria misa, iliyopangwa kufanyika jana katika Shule ya Msingi ya Lake Kenyatta katika mji wa Mpeketoni.
Juzi, Ruto aliyefanya harambee katika majimbo ya Kwale na Kilifi, aliwataka Wakenya kutilia mkazo suala la amani.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4529

Trending Articles