
Meghji ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu, alisema “Mafanikio yoyote ya kiongozi yeyote yanatokana na ushirikiano na upendo kwa wale anaowaongoza. Na mimi mafanikio yangu yametokana na ninyi,” alisema Meghji.
Katika hafla hiyo ya kumzawadia iliyofanyika jijini Dar es Salaam, akizungumzia suala la ujangili, Meghji alisema vita dhidi ya ujangili haitafanikiwa, ikiwa hakutakuwa na ushirikiano mzuri wa kuanzia kwa wafanyakazi wenyewe.
Alisema kwa sasa ujangili wa tembo ni mkubwa na umekuwa tishio na hautazuiwa kwa silaha pekee, bila kuwa na ushirikiano mzuri na elimu kwa wananchi ili waone umuhimu wa kuwalinda wanyama.
Alisema upo umuhimu wa kuwapa motisha wafanyakazi, wanaofanya wanaolinda wanyama, hasa wale wanaoishi porini ili kuwaongezea ari ya kufanya kazi.
Akisoma hotuba kwa Niaba ya Waziri wa Wizara hiyo, Lazaro Nyalandu, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Maimuna Tarishi, alisema Meghji ni kiongozi pekee anayefaa kuigwa, kwani ndiyo Waziri aliyewahi kuongoza wizara hiyo kwa muda mrefu wa miaka tisa.
Alisema Meghji alileta mapinduzi makubwa katika wizara hiyo na kuwezesha mafanikio makubwa, ikiwemo tembo kuongezeka kutoka 120,000 mpaka kufikia 141,000.
“Tunaamini juhudi hizi na mafanikio haya ambayo tuliyonayo leoi hii yanatokana na juhudi zako binafsi za kuwamotisha wafanyakazi na kuwawezesha kwa vitendea kazi,” alisema.