Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4617

MAHARI YAZUA BALAA, BABA WA MTOTO AZUIWA KUZIKA

$
0
0
Familia mbili mjini hapa zimejikuta zikiingia katika uhasama mkubwa, kiasi cha kupigana fimbo na ngumi makaburini katika ugomvi wa kugombea kuzika mwili wa mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.
Sababu kubwa ya mpasuko huo imeelezwa kuwa ni mahari, kwani wazazi upande wa mama wa mtoto huyo walikuja juu na kumzuia baba wa mtoto, Joseph Bacho mkazi wa Mtaa wa Kawajense- Madukani   mjini  hapa asishiriki katika shughuli zozote za maziko ya mtoto wake wakidai hawamtambui kwa kuwa hajatoa mahari kwa binti yao.
Inaelezwa kuwa, Joseph  na mzazi  mwenzake,  Anna Kizo ambaye pia ni mkazi  wa Mtaa wa Kawajense –Madukani  walimzaa mtoto  Junior Bacho nje  ya ndoa  ambapo  hadi  umauti unamfika  mtoto  huyo, baba yake  mzazi  alikuwa  hajajitambulisha  kwa  upande wa mwanamke wala kutoa mahari.
Na kwamba, tangu kuzaliwa kwa mtoto huyo, alikuwa akiishi na kulelewa na  mama  yake mzazi, Anna  nyumbani kwa wazazi wake katika Mtaa  wa Kawajense.
Kwa mujibu wa waombolezaji ambao hata hivyo hawakuwa tayari kutajwa majina, vurugu hizo ziliibuka baada ya upande wa ndugu wa baba wa mtoto kuweka msiba nyumbani kwao na kuandaa taratibu za kumzika mtoto huyo.
Hata hivyo, kitendo hicho kilipingwa na upande wa mama wa mtoto, ukisema ndio wenye haki ya kumzika mtoto huyo ambaye hawakuwahi kumtambua kisheria baba yake mzazi.
Ndugu wa upande wa baba ulifanikiwa kuchimba kaburi, kuutoa mwili mochari na kuufikisha nyumbani tayari kwa maziko, lakini vurugu za upande wa pili ikiwa pamoja na ndugu upande wa mama kufukia kaburi, zilisimamisha shughuli zote, huku malumbano yakishika hatamu hadi askari wa jeshi la polisi kupitia kikosi chake cha kuzuia fujo (FFU) kilipolazimika kuingilia kati na kusimamia shughuli za kuurudisha mwili katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda.
Inaelezwa kitendo cha upande wa mama wa mtoto kufukia kaburi ndiko kulikochangia kuchochea vurugu hadi FFU walipoingia kati.
Kamanda  wa Polisi  wa Mkoa  wa Katavi, Dhahiri Kidavashari  amethibitisha kutokea  kwa mkasa huo  kwamba  hakuna  mtu  yeyote aliyejeruhiwa katika  vuta nikuvute  hiyo  pia  hakuna  ayekamatwa  kuhusiana na tukio hilo  ambalo ni la kijamii  zaidi.
Mkasa mzima unadaiwa kutokea mtaani hapo Alhamisi wiki hii, siku ambayo mtoto huyo alifariki dunia katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda alikokuwa akiuguzwa na shangazi yake, Evelyne Komba na bibi yake mzaa baba, Teddy Francis.
Inaelezwa kuwa, wakiamini wana haki zote za kumzika mtoto huyo, waliuchukua mwili na kuweka msibani nyumbani kwao, jambo lililopingwa na upande wa mama wa mtoto waliokuja juu na kusema hawamtambui baba wa mtoto kwa kuwa hakuwa ametoa mahari.
“Ujue  katika  mila na desturi  zetu  mtu  kama  amezaa na  msichana  bila kuoana  huwa hatambuliwi  na  upande wa mzazi  wa kike  mpaka  atakapolipa mahari  hapo  ana kuwa na haki  zote  kwa  mwanae …sasa kwa upande  wa Joseph  amezaa  tu  na binti  yetu  nje ya ndoa  hivyo  hatumtambui  mpaka  aje ajitambulishe  na  kulipa  mahari.
“Kwa  utaratibu  huo  Joseph  hana  kabisa  haki  ya  kuweka msiba  wa mjukuu  wetu  wala kumfanyia  maziko  mpaka  akamilishe  taratibu zote za mila na desturi  zetu  ikiwemo  kulipa  mahari  kwa wakwe zake “ alisisitiza mmoja  wa  wanandugu  upande  wa  mama mzazi  wa marehemu .
Licha ya kurushiana maneno  makali  pande  hizo  mbili,  upande wa  ndugu wa  baba mzazi  wa marehemu  waliibuka  na  kumshutumu  mama  na  ndugu zake kushindwa  kumhudumia  mtoto  huyo  wakati alipougua .
Inadaiwa mama  wa marehemu  hakumruhusu kabisa  mzazi mwenzake  kumwona mwanae  alipokuwa   mgonjwa  na kuuguzwa  nyumbani  kwa mama yake  katika Mtaa wa  Kawajense – Madukani  .
“Joseph kila  alipofika  nyumbani  kwa mzazi  mwenzake  ili  kumjulia  hali mwanae  aliyekuwa mgonjwa  hakuruhusiwa kuingia  ndani  kwa mdai  kuwa mtoto alikuwa  amelala  “  anadai  mtoa  taarifa .
Inadaiwa  Joseph  aliamua kumchukua mwanae  huyo Juni  18 , mwaka huu   kwa  nguvu kutoka kwa mama  yake  mzazi  na kumpeleka  hospitalini  alikolazwa kwa  matibabu  baada ya kubainika kuwa  anasumbuliwa na utapia mlo mkali .
Kwa mujibu  wa  mashuhuda  ndipo  upande  wa  ndugu  wa mama mzazi  wa marehemu  walipozira   ikidaiwa kuwa  hawakuweza kufika  hata siku  moja  kumjulia  hali  mtoto  huyo aliyekuwa akiuguzwa  hospitalini hapo  na shangazi  yake Evelyne na  bibi  yake Teddy  hadi  umauti  ulipomfika .
Licha  ya upande  wa  ndugu wa mama mzazi  wa marehemu  kushushiwa  tuhuma na  lawama  hizo  nzito  waliendelea  na msimamo  wao   kwamba walikuwa na  haki ya  kumzika marehemu  hivyo nao  wakaamua kuweka msiba  nyumbani  kwa mama wa marehemu  katika Mtaa  huo  wa Kawajense.
Ndipo juzi , Juni 27 wazee  wa Mtaa  wa Kawajense  waamua kuingilia kati mgogoro  huo  kwa  kuzikutanisha pande  hizo  mbili  zilizokuwa  zikivutana na kufikia uamuzi  kuwa  msiba  uwe nyumbani  kwa  baba  wa marehemu.
Kufutia uamuzi huo shangazi wa marehemu aliongoza ndugu  zake akiwemo  baba mzazi  wa marehemu  hadi  chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali  ya  wilaya ya Mpanda mjini hapa  na kuuchukua mwili wa marehemu kisha kuupeleka nyumbani  kwa  bibi  ya marehemu  kwa ajili  ya maandalizi  ya maziko  yake .
Maziko  ya mtoto  huyo  yalipangwa  kufanyika  katika makaburi  ya Kawajense –Msufini  ambako  upande  wa ndugu wa baba mzazi  wa marehemu walichimba  kaburi katika eneo  hilo,  lakini muda mfupi  baada ya kukamilisha  kuchimba  kaburi  hilo  ndugu  wanaodaiwa  wa upande wa mama  mzazi  wa marehemu waliwawavamia  wachimba  kaburi na kuwalazimisha kulifukia .
Waombolezaji  waliokuwa msibani  nyumbani  kwa bibi ya marehemu baada ya kutaarifiwa  tukio hilo lililotokea makaburini  walitimua mbio  na kuelekea makaburini  na kukuta baadhi ya wanandugu upande wa mama wakimalizia kufukia  kaburi  hilo.
Walipoulizwa sababu za kufukia kaburi hilo,  walianza kufoka ndipo inadaiwa  kundi la ndugu wa mama wa marehemu  waliibuka na  kuanza kuwashambulia kwa kuwacharaza fimbo  ndugu wa baba mzazi  wa marehemu .
Hadi  sasa  mwili  wa mrehemu  huyo umehifadhiwa  mochari  katika Hospitali  ya Wilaya ya Mpanda  hadi  hapo  pande  hizo  mbili  zinazovutana zitakapoafikiana  ndipo  ufanyiwe maziko .

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4617

Trending Articles