Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Li Yuanchao alitembelea Hifadhi ya Ngorongoro na kuisifia Tanzania kwa jinsi inavyosimamia masuala ya uhifadhi wa wanyamapori.
Kiongozi huyo wa China alitua nchini kupitia Uwanja Mdogo wa Arusha juzi jioni katika zira yake ya siku sita nchini, akitokea Zambia.
Akiwa amefuatana na ujumbe wa China, Yuanchao alipokelewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na viongozi mbali wa Serikali ya Tanzania akiwemo Waziri wa Nchi, Utawara Bora, George Mkuchika na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo.
Makamu huyo wa Rais wa China alipata fursa ya kutembelea kreta akiwa katika hifadhi hiyo, ambayo ni kivutio muhimu nchini.
Bonde la Ngorongoro ambalo ni maarufu duniani ndiyo sehemu pekee katika Afrika na duniani kote, ambako wanyama pori na binadamu wanaishi pamoja kwa amani bila shida yoyote.
Eneo la Kreta ya Ngorongoro au Bonde la Ngorongoro, ndilo eneo maarufu na kivutio kikuu cha maelfu ya watalii wanaotembelea Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kila mwaka kutoka kote duniani kwa ajili ya kujifunza na kujifurahisha kwa kuona wanyama wa aina mbalimbali.
Kiongozi huyo wa China alishuka kwenye Kreta ya Ngorongoro na kujionea juu ya umbaji wa Mungu na utajiri wa wanyamapori. Aliitaka Tanzania kuendeleza shughuli za uhifadhi kwa matumizi ya sasa na vizazi vijavyo.
Alisema nchi yake inatambua juhudi ya Tanzania katika shughuli za uhifadhi na mapambano yake juu ya tatizo la ujangili ambalo linatishia uwepo wa wanyamapori. China ni mdau mkubwa wa maendeleo nchini Tanzania na katika miaka ya hivi karibuni idadi ya watalii kutoka China imekuwa ikiongezeka kila mwaka.