Benki ya Exim Tanzania imekabidhi hundi ya Sh milioni 10 kwa Taasisi ya Tushikamane Pamoja (TPF) ikiwa na lengo la kusaidia wazee wasiojiweza wanaoishi katika kaya zaidi ya 40 jijini Dar es Salaam.
Taasisi hiyo ambayo kwa sasa inasambaza chakula na vitu binafsi kwa kaya 40 jijini Dar es Salaam kila mwezi pia hutekeleza miradi mbalimbali ambayo ni pamoja na matibabu kwa kundi hilo maalumu.
Akizungumza wakati wa makabidhiano yaliyofanyika jana, Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Madhara na Utekelezaji wa Kanuni wa Benki ya Exim, David Lusala alisema benki inajua umuhimu wa kuchangia sehemu ya pato lake kwa jamii, kwa njia ya miradi ambayo inabadilisha au kuboresha maisha ya kijamii na kiuchumi.
 "Benki ya Exim imekuwa makini sana katika kusaidia jamii inayoizunguka. Kama sehemu ya shughuli zetu za kijamii, leo (jana) tunakabidhi Sh milioni 10 kwa TPF ili kupiga jeki miradi yao iliyoanzishwa ya kusaidia wazee wasiojiweza na jamii kwa ujumla.
Alitaka taasisi hiyo kuhakikisha fedha hizo zinaelekezwa kwenye matumizi yaliyokusudiwa.Â
Mweka Hazina wa Taasisi ya Tushikamane Pamoja, Ana Rupia aliipongeza benki hiyo. Alisema wanao mpango wa kujenga nyumba kwa ajili ya wazee katika eneo la Kwembe, wilayani Kinondoni itakayotoa urahisi kwa kundi hilo kupata huduma za matibabu, usimamizi wa karibu na huduma nyingine za kibinadamu.