Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) wamegoma kusimamia mitihani wakishinikiza malipo ya posho za usimamizi wanazodai tangu muhula wa masomo uliopita.
Mgomo wa wanataaluma hao wa Shule ya Sayansi ya Jamii katika chuo hicho, umeathiri wanafunzi zaidi ya 2,000 waliokuwa wafanye mtihani jana.
Ofisa Uhusiano wa Udom, Beatrice Baltazari alisema wanafunzi wengine wameendelea na mitihani kama kawaida isipokuwa hao wa Sayansi ya Jamii.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, wahadhiri hao wanadai Sh milioni 40 ambazo ni posho za muhula uliopita .
Alisema shule ya Sayansi ya Jamii ina wanafunzi takribani 5,000. Hata hivyo waliokuwa na ratiba ya kufanya mitihani hawakufanya kutokana na mgomo huo.
“Siyo wanafunzi wote 5,000 walikuwa na mitihani leo (jana). Lakini hata hivyo tumekaa na wahadhiri waliogomea kusimamia mitihani na kwenye kikao, chuo kimeahidi kulipa fedha hizo lakini fedha leo hazipo zikipatikana watalipwa madai yao yote. Tunaamini wanafunzi ambao hawakufanya mtihani leo (jana) watafanya mitihani yao,” alisema.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi, baadhi ya wanafunzi walisema wamesikitishwa na hali hiyo ikizingatiwa kwamba, walikuwa wamejiandaa kuanza jana.
Taarifa kutoka chuoni hapo zilidai, licha ya madai ya posho za kusimamia mitihani ambazo hawajalipwa kwa miaka mitatu sasa, pia wanataaluma hao wanadai kuwa na mazingira mabaya ya kufanyia kazi.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho Proesa Idris Kikula alipoulizwa kuhusu mgomo huo, alisema yuko Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.
Hata hivyo, Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho, anayehusika na Mipango, Utawala na Fedha, Profesa Shaban Mlacha alisema wamemaliza kikao na wahadhiri hao na kukubaliana warudi kusimamia mitihani na fedha wanazodai zitalipwa.
“Ni kweli waligoma na tumekaa nao kukubaliana walipwe fedha zao na warudi kusimamia mtihani yao,” alisema Mlacha.