Wasomi wengi nchini wameshindwa kujiajiri kutokana na kutojua kuwa elimu waliyonayo imewafungua akili ili waweze kufanya mambo yao wakiwa na uelewa mzuri hali inayowafanya kutegemea vyeti walivyonavyo.
Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Waziri Ofisi ya Rais asiyekuwa na Wizara Maalumu Profesa Mark Mwandosya alipokuwa kwenye mahafali ya wanafunzi
ambao ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa vyuo vikuu vilivyopo mkoani Dodoma.
Mwandosya alisema wengi wamejikuta wamekwama kujiajiri kutokana na kusubiri ajira bila kujua kuwa elimu waliyopata imelenga kuwasaidia kufanya mambo ya kimaisha kutokana na uelewa walioupata vyuoni na vinginevyo.
Alisema hivi sasa ushindani katika soko la ajira ni mkubwa kutokana na wasomi kuwa wengi hivyo ni afadhali wakaweka malengo ya kujiajiri pindi wanapomaliza masomo yao.
‘’Vijana wangu … hakikisheni mnajiwekea malengo ya kujiajiri pindi muondokapo vyuoni maana kukosa malengo kutawafanya kutojituma na kujikuta kila siku mkiuza vyeti ambavyo kila mtu anavyo badala ya ubora wa elimu mlioupata vyuoni’’, alisema.
Awali chama cha CCM kilipokea jumla ya wanachama wapya 230 na kuwakabidhi kadi wanachuo wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP) na wengine sita waliokabidhi kadi wakitokea Chadema akiwemo kiongozi wao Belina Maingu maarufu kwa jina la Balozi.
Jumla ya wanafunzi 1,500 wa vyuo 10 vilivyopo mkoani hapa ambao ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi walikutana kwenye mahafali ya kwanza yaliyowakutanisha kwa pamoja mwaka huu tofauti na miaka mingine ambayo kila chuo hufanya chenyewe.