Wasomi, wanaharakati na wananchi kwa ujumla wamepongeza Bajeti ya mwaka 2014/15 ya Sh trilioni 19 iliyowasilishwa bungeni juzi na kujikita zaidi katika kuimarisha miundombinu ya elimu, usafiri wa reli na usambazaji wa nishati ya umeme vijijini, wakisema imekata kiu ya Watanzania wengi.
Aidha, wamepongeza hatua ya kuondoa misamaha ya kodi katika maeneo muhimu na kusema hali hiyo inaonesha kuimarika kwa wizara hiyo katika suala la kuhakikisha taifa linakua kiuchumi.
Akizungumza na gazeti hilo jijini Dar es Salaam jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Benson Bana alisema maandalizi ya bajeti ya mwaka huu yanaonesha yaliandaliwa vizuri na kwamba wameangalia jinsi ya kugharimia bajeti ya maendeleo kwa kutumia vyanzo vya ndani.
Dk Bana alisema, kikubwa kinachofurahisha katika bajeti hiyo ni kwamba Wizara imeangalia mambo muhimu na kuyatengea bajeti ambapo kwa upande wa bajeti ya maendeleo, Serikali imeainisha vyanzo vya ndani katika kupata fedha za bajeti hiyo, badala ya kutegemea fedha kutoka kwa wahisani.
“Ni jambo zuri na tunapaswa kuwapongeza Serikali kwa kuona hili, inaonesha Wizara imeimarika na walijiandaa,” alisema Dk Bana.
Akizungumzia kuhusu kupunguza misamaha ya kodi, Dk Bana alisema ni jambo jema kwa wizara kuona haja ya kufanya hivyo kwani, baadhi ya misamaha iliyokuwa ikitolewa haikuleta tija kwa maendeleo ya taifa.
Alisema hatua hiyo hivi sasa itajenga uwajibikaji na uwazi kwa watendaji wa Serikali kwani kwa watakaosamehewa kodi watatangazwa na kujulikana kama misamaha yao ina tija au la.
Kuhusu, mishahara na vipaumbele vya Serikali, Dk Bana alisema kuweka vipaumbele ni jambo jema ambapo kwa kuangalia hili Serikali imetenga jumla ya Sh trilioni 3.4 kwenye sekta ya elimu ambayo ndiyo imetengewa fedha nyingi kuliko zote.
Alisema jambo hilo litaisadia kuboresha sekta hiyo ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikilalamikiwa na kuonya kuwa ni vyema wanaopata mikopo ya masomo kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, mara wamalizapo warudishe mkopo waliopewa.
“Tujenge tabia ya kulipa, ili na wengine wakopeshwe. Umepewa mkopo umesoma umemaliza una kazi au huna kazi, lakini angalia jinsi ya kurejesha mkopo ili wengine nao wasome,” alisisitiza Dk Bana.
Pamoja na kusifu bajeti hiyo, Dk Bana aliikosoa kwa kusema haikuonesha vyanzo vipya vya mapato na kusisitiza kwamba Serikali ingekuwa na mtazamo wa kuangalia sekta na watu binafsi kuona mchango wao katika pato la Taifa ni upi na kama wanalipa kodi inavyostahili.
Alisema ni vyema hata posho za wabunge zingepaswa kukatwa kodi ili kupata chanzo kipya cha kodi na pia hata ruzuku za vyama vya siasa nazo zingekuwa zinakatwa kodi.
Alisema kufanya hivyo kuwaongeza vyanzo vya fedha na kupunguza mzigo mzito kwa wananchi hasa wa kodi na ushuru kwenye bidhaa za lazima kama vile, saruji, mabati na mafuta ambazo zinapoongezeka kodi zinaathiri maisha ya wananchi wengi hususan wa vijijini.
Naye Mtaalamu wa Uchumi ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Haji Semboja alisema kupungua kwa makato ya kodi ni jambo zuri na la heri kwa kuwa itaongeza vipato kwa wananchi wenye ajira. Pia alisema uamuzi wa serikali na taasisi zake kuagiza vifaa kwa pamoja ni jambo jema kwani litapunguza mianya ya rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dk Hellen Kijjo Bisimba alisema pamoja na mipango mizuri ya Serikali kwenye bajeti hiyo, lakini haikuja na vyanzo mbadala vya mapato.
Alisema kuendelea kuongeza kodi kwenye vileo kama vile pombe na sigara, vinaweza kuathiri familia nyingi ambapo wazazi au walezi wa familia hizo nao watapunguza kiwango cha fedha za matumizi ya nyumbani ili kubaki na fedha za vileo.
“Kama awali baba au mama alikuwa anaacha Sh 10,000 ya matumizi kwa siku nyumbani hivi sasa itabidi aache 8,000 ili abakiwe na fedha kwa ajili ya kileo na sigara ambavyo vimeongezwa kodi, sasa hii ni kutesa familia,” alisema Dk Bisimba.
Dk Bisimba aliongeza, katika hilo familia ndizo zitapata shida kwa kuwa si rahisi ulevi kwisha na badala yake wataendelea kunywa, lakini kama serikali ingebuni vyanzo vingine vya mapato na kuacha kuongeza kodi kwenye vileo ingekuwa bora zaidi.
Hata hivyo, alisema bajeti ya afya pamoja na kutengewa fedha Sh trilioni 1.5 bado kiwango hicho ni kidogo kwa kulinganisha na makubaliano ya nchi za Afrika Mashariki kuwa asilimia 15 ya bajeti itengwe kwa ajili ya sekta ya afya.
Bajeti kuu ya Serikali ilitangazwa juzi bungeni ya Sh trilioni 19.87 ambayo iliwasilishwa na Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya huku ikiwabana wananchi katika bidhaa na huduma za starehe huku ikitoa kipaumbele kwenye sekta ya elimu.
Kwa upande wa Waziri Mkuu mstaafu, Dk John Malecela alisema bajeti ya mwaka huu imekuwa na mambo mengi muhimu yaliyokuwa yakihitajika kwa wananchi.
Pongezi nyingine zimetoka kwa Mbunge wa Jimbo la Hai na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliyesema bajeti imezingatia mambo muhimu ikiwa pamoja na kupunguza misamaha ya kodi, jambo alilosema ni la maana. Lakini alinung’unikia punguzo dogo la kodi wanayotozwa wafanyakazi katika mishahara, punguzo la asilimia moja kutoka 13 hadi 12 bado ni ndogo, hivyo linapaswa kupungua zaidi.
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi (TUCTA), Nicholas Mgaya alisema pamoja na punguzo la kodi katika mishahara, bado serikali inapaswa kuendelea kushusha na kufikia digiti moja, yaani chini ya asilimia 10.
Aidha, alisema ahadi ya kuongeza kima cha chini cha mishahara kwa watumishi wa umma itakuwa hatua nzuri kutokana na kile alichosema kiwango cha mshahara wanaolipwa hauendani na hali halisi ya maisha ya Mtanzania kwa sasa.
Kwa ujumla, wananchi wengi waliozungumza na gazeti hili walielezea kufurahishwa na bajeti, hasa kwa uamuzi wa kufyeka misamaha ya kodi wakisema itasaidia kuongeza kukuza uchumi wa nchi, hivyo kuchochea kasi ya maendeleo na pia kupunguza makali ya maisha.