Polisi Mkoa wa Kinondoni, imewakamata vijana wawili wanaodaiwa kujifanya waganga wanaotoa tiba kwa wanawake, ambayo masharti yake ni kushiriki nao ngono bila kinga na kuacha nguo za ndani, ili zifanyiwe dawa zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Englibert Kiondo, alidai vijana hao Juma Hemedi (32) na Abrahman Mulsin, wote wakazi wa Tandika, baada ya kushiriki ngono na wagonjwa wao huwaambia waache nguo za ndani.
Kamanda Kiondo alidai baada ya kupata malalamiko, Jeshi la Polisi lianzisha msako na kuwapekua waganga hao, ambapo walikutwa na nguo za ndani za kike 22, ambazo alisema zitakuwa ushahidi wa kuingiliwa kimwili kwa wanawake hao. Vitu vingine wanavyodaiwa kukutwa navyo ni pembe, tunguli, makopo ya dawa na vibuyu.
“Sheria iko wazi, inasema mganga anapofanya ngono kama uganga anakuwa amebaka, na hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu 130 sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002,” alisema Kamanda Kiondo.
Kwa mujibu wa madai ya Kamanda Kiondo, vijana hao wamekuwa wakijifanya waganga wa tiba asili, husambaza vipeperushi sehemu mbalimbali za jiji kutafuta wateja.
Mbali na tiba hiyo ya kupata watoto, inayotolewa kwa kushiriki ngono na mganga, Kamanda Kiondo alidai watuhumiwa hao wamekuwa wakidai kutibu magonjwa mengine kama kisukari, vidonda vya tumbo, nguvu za kiume, kukuza maumbile, kupata kazi, kufaulu mtihani, mvuto wa biashara, kumilikishwa jini na kupewa pete ya bahati.